Iran na Tanzania kupanua ushirikiano wa karantini na kilimo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136694-iran_na_tanzania_kupanua_ushirikiano_wa_karantini_na_kilimo
Mkuu wa Shirika la Ulinzi wa Mimea la Iran ameeleza azma ya taifa hili ya kukuza ushirikiano na Tanzania katika uga wa karantini na kilimo.
(last modified 2026-02-16T10:18:12+00:00 )
Feb 16, 2026 10:18 UTC
  • Iran na Tanzania kupanua ushirikiano wa karantini na kilimo

Mkuu wa Shirika la Ulinzi wa Mimea la Iran ameeleza azma ya taifa hili ya kukuza ushirikiano na Tanzania katika uga wa karantini na kilimo.

Maryam Jalili-Moghadam, Mkuu wa Shirika la Ulinzi wa Mimea la Iran, ametangaza mipango ya Tehran ya kupanua ushirikiano wa kilimo na karantini kati yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkuu wa Shirika la Uhifadhi wa Mimea la Iran amesisitiza umuhimu wa kuimarisha maingiliano katika kupambana na wadudu wa mazao, kubadilishana ujuzi wa kiufundi, na kurahisisha biashara ya bidhaa za kilimo baina ya mataifa hayo mawili.

Maryam Jalili-Moghadam amesema hayo katika mazungumzo yake na Azim Dewji mfanyabiashara na mwanaharakati wa masuala ya uchumi kutoka Tanzania na kusisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamuu ya Iran inataka kukuza mahusiano ya kibiashara, hasa katika kilimo, na nchi marafiki kama Tanzania.

Aidha ameongeza kwamba kwa kuzingatia madhara ya pamoja ya wadudu wa pamoja kama panzi wa jangwani na uanachama wa pande zote mbili katika Mkataba wa Kimataifa wa Kuhifadhi wa Mimea, kunaweza kufanywa mafunzo ya pamoja na makubaliano ya karantini.

Maryam Jalili-Moghadam alibainisha kuwa uhamishaji wa teknolojia mpya za ufuatiliaji na utambuzi wa wadudu, pamoja na mafunzo ya karantini, utaongeza uwezo wa kitaalamu kwa pande zote mbili.

Pia alitaja kurahisisha biashara ya kilimo kama lengo lingine la ushirikiano huu, akisema kwamba kukubalika kwa pande zote kwa vyeti vya karantini kunaweza "kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa kibali cha kuruhusu bidhaa katika forodha na gharama za biashara." Kuendeleza usafirishaji na uagizaji wa dawa za kuulia wadudu na kupanua kilimo cha Iran cha pwani nchini Tanzania pia ni maeneo mengine yaliyosisitizwa katika mkutano huo.