Afrika Kusini: Ramaphosa atangaza kutumwa jeshi kukabiliana na jinai
-
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini
Katika jitihada za kupunguza viwango vya juu vya magenge ya uhalifu na jinai nyingine, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametangaza kuwa atatuma jeshi ili kushirikiana na polisi katika suala hilo.
Rais wa Afrika Kusini jana alieleza kuwa jinai zilizoratibiwa hivi sasa ni tishio la haraka zaidi kwa demokrasia ya nchi hiyo, jamii na maendeleo ya kiuchumi. "Lengo letu kuu mwaka huu ni kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya jinai zilizoratibiwa na magenge ya uhalifu,'' ameeleza Rais Ramaphosa.
Ameongeza kuwa, Afrika Kusini haiwezi kupambana na watenda jinai kwa kuamiliana nao kwa upole. "Ni lazima tuchukue hatua kali na kutekeleza kikamilifu sheria. Ningependa ujumbe huu uwe wazi, hakutakuwa na kinga kwa vitendo vya uhalifu na ufisadi."
Amesema, Afrika Kusini inafanya jitihada nyingine kukabiliana na uhalifu ikiwa ni pamoja na kuajiri maafisa wapya wa polisi 5,500. Amesema inashangaza kuona kuwa karibu watu 60 huawa kila siku nchini Afrika Kusini.
Vifo hivyo ni pamoja na wale wanaouliwa katika mapigano kati ya magenge ya mihadarati na uhalifu wa kutumia silaha unaohusiana na biashara haramu ya uchimbaji madini.