"Ni muhali kufikia amani na Israel madhali inakiuka haki za Wapalestina"
Waziri wa Mambo ya Nje na Wahamiaji wa Palestina, Varsen Aghabekian Shahin amesema kufikia amani na Israel "haiyumkiniki" madhali haki za Wapalestina zinakiukwa na utawala huo wa Kizayuni, akisisitiza kwamba sheria za kimataifa zinapasa kuzingatiwa, na uchukuaji wa hatua za upande mmoja lazima ukomeshwe.
"Amani na Israel katika mazingira ya sasa ya ukiukwaji wa mara kwa mara wa haki za Wapalestina haiwezekani," Shahin amesema pambezoni mwa Mkutano wa Usalama wa Munich Jumapili.
Amebainisha kuwa, hatua za upande mmoja za Israel katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni pamoja na Ukingo wa Magharibi na Quds Mashariki, sanjari na upanuzi wa makazi ya walowezi wa Kiyahudi kinyume cha sheria, zinazuia fursa na uwezekano wa kufikiwa azimio la mazungumzo.
"Kila kitu ambacho Israel inafanya kwa upande mmoja katika maeneo yanalokaliwa kwa mabavu kinapaswa kuzingatiwa kuwa batili," Shahin amesema, akisisitiza kwamba unyakuzi wa ardhi za Wapalestina "ni ukiukaji wa sheria za kimataifa, na ni uhalifu unaofaa kusimamishwa."
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Palestina pia ameashiria makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yaliyoanza Oktoba 10, akisema kwamba kusonga mbele hadi awamu ya pili, kunategemea kufuatwa kikamilifu makubaliano ya awali.
Waziri wa Mambo ya Nje na Wahamiaji wa Palestina amesema, "Tunachotaka ni ulimwengu kusimama na kuzungumza. Kutazama tu, kumetosha. Sheria za kimataifa ziko wazi sana,'" amesema, akirejelea maamuzi ya kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa ambayo yanaona ujenzi wa makazi mapya na uporaji wa ardhi za Palestina kuwa kinyume cha sheria.