ANC yamkosoa Mfalme wa Afrika Kusini kwa kuwaalika maafisa wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136250-anc_yamkosoa_mfalme_wa_afrika_kusini_kwa_kuwaalika_maafisa_wa_israel
Chama tawala cha African National Congress (ANC) kimemkosoa vikali Mfalme wa Afrika Kusini, Buyelekhaya Dalindyebo kufuatia uamuzi wake tata wa kuwaalika maafisa kutoka Ubalozi wa Israel kutembelea hospitali za umma katika mkoa wa Eastern Cape. Dalindyebo ni mfalme wa watu wa AbaThembu, mojawapo ya jamii kubwa zaidi za kitamaduni za Afrika Kusini.
(last modified 2026-02-04T10:23:14+00:00 )
Feb 04, 2026 10:23 UTC
  • ANC yamkosoa Mfalme wa Afrika Kusini kwa kuwaalika maafisa wa Israel

Chama tawala cha African National Congress (ANC) kimemkosoa vikali Mfalme wa Afrika Kusini, Buyelekhaya Dalindyebo kufuatia uamuzi wake tata wa kuwaalika maafisa kutoka Ubalozi wa Israel kutembelea hospitali za umma katika mkoa wa Eastern Cape. Dalindyebo ni mfalme wa watu wa AbaThembu, mojawapo ya jamii kubwa zaidi za kitamaduni za Afrika Kusini.

Mwaliko huo umezusha hasira, hasa kutokana na msimamo wa kihistoria wa ANC dhidi ya ubaguzi wa rangi na kujitolea kwake kuunga mkono Palestina katika kukabiliana na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Baada ya kumalizika mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho ngazi ya mkoa (PEC), maafisa wa ANC walielezea kusikitishwa kwao na hatua ya mfalme huyo, wakimtaja kama kiongozi aliyesaliti kanuni ambazo mababu zake walipigania wakati wa Mapambano ya Ukombozi wa Afrika Kusini.

Hisia hizi za hasira ziliungwa mkono na shakhsia muhimu ndani ya chama, akiwemo Mwenyekiti wa ANC katika mkoa wa Eastern Cape, Oscar Mabuyane, Katibu Mkuu wa chama mkoani hapo, Lulama Ngcukayitobi, na Msemaji wa chama, Yanga Zicina. Ngcukayitobi amemtaka mfalme huyo kutafakari kuhusu tabia yake ya hivi karibuni, akisema amewaathiri watu wake na serikali nzima ya Afrika Kusini, ambayo msimamo wake wa tangu jadi ni kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya watu wa Palestina.

Haya yanaripotiwa, chini ya wiki moja baada ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israel na Afrika Kusini kuingia katika mgogoro mkubwa na usio wa kawaida, baada ya pande zote mbili kutangaza maafisa wa kidiplomasia wa kila upande kuwa watu wasiofaa na kuwaamuru waondoke ndani ya saa 72. Hatua hiyo ya Ijumaa iliyopita inatambuliwa kuwa kilele cha mvutano unaoendelea kati ya pande hizo mbili, hasa baada ya vita vya Israel na mauaji ya kimbari ya utawala huo dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, na vilevile hatua ya Afrika Kusini ya kuifungulia Israel mashtaka katika mahakama za kimataifa kwa mauaji ya Wapalestina.

Mgororo wa kidiplomasia baina ya pande hizo mbili ulishadidi baada ya Afrika Kusini kuwasilisha mashtaka dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ huko mjini The Hague, tarehe 29 Desemba 2023, ikiutuhumu utawala huo wa Kizayuni kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.