Somalia kuanza kutoa pasipoti za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
-
Mustafa Ahmed Dhuhulow, Abdullahi Sheikh Ismail na Ilyas Ali Hassan, pichani kwa utaratibu
Somalia inatarajiwa kuanza kutoa hati ya kusafiria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa raia wake; ikiungana na nchi nyingine wanachama katika kutumia hati ya kusafiria ya kikanda.
Ilyas Ali Hassan Balozi wa Somalia nchini Tanzania na Mwakilishi wa Kudumu wa nchi hiyo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) leo Jumanne alikabidhi nchini Tanzania vipengele rasmi vya muundo wa pasipoti za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Somalia Jenerali Abdullahi Sheikh Ismail “Fartaag” na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uhamiaji na Masuala ya Uraia la nchi hiyo Mustafa Sheikh Ahmed Dhuhulow.
Hatua hii inaashiria hatua muhimu ya kidiplomasia kwa Somalia na inatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuwezesha harakati huru za raia wa Somalia katika eneo la Afrika Mashariki.
Somalia ilipata idhini rasmi ya kuchapisha pasipoti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mwezi Desemba 2025, kabla ya wiki hii kuwasilisha vipengele vilivyoidhinishwa vya muundo wa hati hiyo ya kusafiria.
Pasipoti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ilitambulishwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa 17 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya hiyo Machi 2, 2016, ambapo viongozi wa EAC walizindua Pasipoti ya Kielektroniki ya Afrika Mashariki katika makundi matatu -yaani Diplomasia, Huduma na Kawaida.
Pasipoti hiyo ya Kielektroniki inayotambulika kama hati ya kimataifa ya kusafiria, imechukua nafasi ya hati za kusafiria za zamani za nchi wanachama wa EAC.
Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Muohamud (kulia) mwezi Machi mwaka 2024 alisaini mkataba wa kujiunga nchi yake na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika hafla iliyofanyika jijini Kampala, Uganda.
Somalia nchi inayopatikana katika eneo la Pembe ya Afrika inajivunia ukanda wa pwani mrefu zaidi barani Afrika wa zaidi ya kilometa elfu tatu. Eneo hilo linaweza kutumiwa kama rasilimali ya kukuza uchumi wa bluu na kuongeza biashara ya kikanda ndani ya nchi wanachama wa EAC.