Utumwa, ukoloni; Ghana yataka nchi za AU kuunga mkono Azimio la Algiers
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136690-utumwa_ukoloni_ghana_yataka_nchi_za_au_kuunga_mkono_azimio_la_algiers
Rais wa Ghana ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kuunga mkono rasimu ya azimio lenye lengo la kutambua dhulma za kihistoria zilizosababishwa na biashara ya utumwa wa kuvuka Atlantiki.
(last modified 2026-02-16T10:14:09+00:00 )
Feb 16, 2026 10:14 UTC
  • Utumwa, ukoloni; Ghana yataka nchi za AU kuunga mkono Azimio la Algiers

Rais wa Ghana ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kuunga mkono rasimu ya azimio lenye lengo la kutambua dhulma za kihistoria zilizosababishwa na biashara ya utumwa wa kuvuka Atlantiki.

John Dramani Mahama ametoa mwito huo akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa Mkutano wa 39 wa AU huko Addis Ababa, Ethiopia.

Mahama amesema kwamba, ingawaje hatua hiyo haitafuta yaliyopita, lakini itakiri rasmi kwamba biashara ya watumwa wa Kiafrika na utumwa kwa misingi ya rangi ya ngozi zilikuwa uhalifu mkubwa ambao ulikuwa na nafasi kuu katika kuunda ulimwengu wa kisasa.

"Watu wote wenye asili ya Kiafrika wamekuwa wakingojea siku hii. Ukweli hauwezi kuzikwa. Misingi ya kisheria ni thabiti; sharti la kimaadili haliwezi kupingwa," amesema Rais wa Ghana.

Kikao cha 39 cha kawaida cha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) kilichofanyika Jumapili jijini Addis Ababa kimepitisha “Azimio la Algiers” kuhusu uhalifu wa kikoloni barani Afrika, huku pia kikiidhinisha tarehe 30 Novemba kuwa Siku ya Afrika ya Mashahidi wa Bara Afrika.

Viongozi wa Afrika waliamua kuitambua tarehe 30 Novemba kama siku ya kuwakumbuka mashahidi na waathiriwa wa biashara ya utumwa wa kuvuka Atlantiki, ukoloni, na mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid), wakisisitiza kuwa kumbukumbu ya pamoja ni msingi muhimu wa utambuzi wa haki, kupatikana kwa uadilifu, na kuzuia kukaririiwa kwa uhalifu kama huo katika siku zijazo.