Raia 16 wauawa katika shambulio jipya la waasi mashariki mwa Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140120-raia_16_wauawa_katika_shambulio_jipya_la_waasi_mashariki_mwa_kongo
Rais wasiopungua 16, wakiwemo wachimbaji madini, wameuawa katika shambulio la hivi karibuni la waasi wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) katika kijiji kimoja mkoani Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2026-07-24T02:48:00+00:00 )
Jul 24, 2026 02:45 UTC
  • Raia 16 wauawa katika shambulio jipya la waasi mashariki mwa Kongo

Rais wasiopungua 16, wakiwemo wachimbaji madini, wameuawa katika shambulio la hivi karibuni la waasi wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) katika kijiji kimoja mkoani Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Janvier Kinyongi, afisa katika eneo la Mambasa alisema jana alipozungumza na waandishi wa habari mjini Bunia, kwamba shambulio hilo lilifanywa mchana wa Jumatano katika kijiji cha Mandeite, katika eneo hilo, umbali wa kilomita 165 (takriban maili 102) kusini-magharibi mwa Bunia makao makuu ya mkoawa Ituri.

"Wengi kati ya waliouawa ni wachimbaji dhahabu. Idadi ya vifo iliyotangazwa ni ya awali kwa kuwa mashambulizi bado yanaripotiwa katika maeneo ya karibu," ameeleza Kinyongi alipozungumza na vyombo vya habari jana.

Shambulio hilo limeripotiwa zikiwa zimepita siku chache tu baada ya watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa ADF kuteka nyara raia kadhaa katika eneo hilo hilo la Mambasa kusini magharibi mwa Bunia.

Waasi wa ADF wanaendelea kuwa tishio kubwa kwa raia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Waasi hao mwezi Juni mwaka huu waliua raia 62 na kuwateka nyara wengine 57. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Ufuatiliaji Usalama la Kivu.

Kundi la ADF, ambalo linalofanya hujuma na uhalifu mashariki mwa Kongo kwa miaka kadhaa sasa lina uhusiano na kundi la wanamgambo la ISIS (Daesh).

Tangu mwaka wa 2021, vikosi vya jeshi la Uganda na Kongo vimekuwa vikifanya operesheni za pamoja dhidi ya ADF.

Katika ripoti ya mwezi Mei, Shirika la Amnesty International ilisema kuwa ingawa kundi la ADF hushambulia vikosi vya usalama, shabaha yake kuu katika miaka ya hivi karibuni imekuwa raia wa kawaida—si tu kwa ajili ya kuiba chakula, dawa na vifaa vingine-, bali pia kama hatua ya kulipiza kisasi kwa operesheni za kijeshi.