Kiongozi Muadhamu amjibu Trump na kusema, Meli za kivita zinaweza kuzamishwa baharini
-
Ayatullah Seyyed Ali Khamenei
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amejibu vitisho vya mara kwa mara vya kijeshi kutoka Marekani dhidi ya Iran, akisema kuwa silaha zenye uwezo wa kuzamisha manowari za Marekani ni “hatari zaidi” kuliko meli hizo za kivita zenyewe.
Akizungumza Jumanne jijini Tehran alipohutubia maelfu ya wananchi kutoka Mkoa wa Azarbaijan Mashariki, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei amesema:
“Rais wa Marekani [Donald Trump] mara kwa mara anadai kuwa jeshi lao ndilo lenye nguvu zaidi duniani. Hata hivyo, hata jeshi linalodaiwa kuwa na nguvu zaidi linaweza kupigwa kwa namna ambayo haliwezi tena kusimama.”
Ameongeza kuwa: “Wanasema mara kwa mara kwamba, ‘Tumetuma manowari kuelekea Iran.’ Sawa—bila shaka manowari inayobeba ndege za kivita ni kifaa hatari. Lakini kilicho hatari zaidi kuliko manowari hiyo ni silaha yenye uwezo wa kuizamisha hadi chini ya bahari.”
Ayatullah Khamenei pia ameashiria kauli za Trump kwamba Washington haijaweza kuupindua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kipindi cha miaka 47, akisema kuwa hilo ni kukiri kufeli kwa njama hizo. Amesema:
“Kwa miaka 47, Marekani imeshindwa kuangamiza Jamhuri ya Kiislamu,” kisha akamhutubu Trump na kuongeza: “Ninasema wazi: hamtaweza kufanya hivyo hata siku zijazo.”
Onyo hilo linakuja wakati Rais wa Marekani, Donald Trump, akiendelea kupeleka vikosi vya kijeshi katika eneo la Asia Magharibi karibu na Iran, huku akitishia mashambulizi dhidi ya nchi hiyo.
Maafisa wa Marekani walisema tarehe 12 Februari kwamba Wizara ya Vita (Pentagon) ilikuwa inatuma manowari nyingine ya kubeba ndege katika eneo hilo, pamoja na maelfu ya wanajeshi, ndege za kivita, na meli za kivita zenye makombora.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameashiria pia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea kati ya Tehran na Washington.
Amesema: “Kauli hizi anazotoa rais wa Marekani—wakati mwingine vitisho, wakati mwingine masharti ya nini kifanyike au kisifanyike—zinaonyesha wazi kuwa wanataka kulitawala taifa la Iran.”
Akifafanua ameongeza: “Wanasema, ‘Hebu tujadili nishati yenu ya nyuklia,’ lakini matokeo ya mazungumzo hayo tayari yameamuliwa: kwamba msibaki tena na nishati hiyo. Kuamua matokeo kabla ya mazungumzo hata kuanza ni kosa na ni upumbavu.”
Amesema pia: “Hii ndiyo njia ya kipumbavu inayofuatwa na marais wa Marekani, maseneta fulani, rais wa sasa, na wengine.”
Hata hivyo, Kiongozi Muadhamu amesema: “Wananchi wa Iran wanaifahamu vyema misingi ya Kiislamu na Kishia,” kisha akanukuu kauli ya Imam Hussein (AS) aliyesema:
‘Mtu kama mimi hawezi kamwe kutoa utii kwa mtu kama Yazid.’
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: “Kwa hakika, taifa la Iran linasema jambo hilo hilo: taifa lenye utamaduni huu, historia hii, na thamani hizi za juu haliwezi kamwe kutoa utii kwa watu wafisadi kama walioko madarakani Marekani leo.”
Katika sehemu nyingine, Ayatullah Khamenei amesema taifa linaomboleza baada ya ghasia za hivi karibuni zilizoungwa mkono na tawala za kigeni, ambazo zilisababisha vifo vya maelfu ya watu.
Ameongeza: “Tuko katika maombolezo kwa damu iliyomwagika.”
Aliwagawanya waliouawa katika makundi matatu.
Kundi la kwanza ni walinzi wa usalama na afya, wakiwemo polisi, wanachama wa Basij, Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), na wengine, aliowataja kuwa “mashahidi wa daraja ya juu.”
Kundi la pili ni raia waliokufa bila hatia wakati wa machafuko.
“Nao pia ni mashahidi,” amesema, akisisitiza kuwa waliuawa katika mazingira ya “fitna ya adui.”
Kundi la tatu ni wale waliopotoshwa na kujiunga na ghasia. Akiwaita “watoto wetu,” amesema baadhi yao walimwandikia wakionyesha majuto, na kwamba mamlaka pia imewatambua waliouawa miongoni mwao kama mashahidi.
Isipokuwa vinara wakuu walioungwa mkono na maadui wa kigeni, Ayatullah Khamenei amesema wengine wote wanastahili kuombewa na kusamehewa.