Jeshi la Niger lasema zaidi ya magaidi 70 "wameangamizwa"
Jeshi la Niger limesema kwamba, zaidi ya magaidi 70 "waliangamizwa" kote nchini kati ya Januari 19 na 25, wakiwemo zaidi ya 50 waliouawa katika mashambulizi ya anga yaliyolenga "mikusanyiko ya maadui."
Katika tangazo la kila wiki jana Jumanne kupitia televisheni ya serikali ya Tele Sahel, Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Niger vimesema kuwa, "washukiwa 48 pia walikamatwa kama sehemu ya operesheni za usalama na ujasusi za nchi kavu zilizofanywa."
Operesheni hizo pia zilisababisha uharibifu wa vifaa muhimu vya maadui, na kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wa uendeshaji wa vikundi vyenye silaha, taarifa hiyo imesema.
Haya yanajiri katika hali ambayo, askari polisi wasiopungua 10 wa Niger wameuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia kituo cha polisi huko Assamaka, mji wa jangwani ulio karibu na mpaka na Algeria, kaskazini mwa nchi hiyo.
Eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi limekumbwa na machafuko ya magenge ya wahalifu wenye silaha kwa miaka mingi sasa.
Haya yanaripotiwa huku Niger, Mali na Burkina Faso zikikusudia kuimarisha ushirikiano wa kiusalama chini ya kikosi kipya cha pamoja kwa lengo la kupambana na makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel barani Afrika.
Mara kwa mara, Rais wa Niger, Abdourahamane Tchiani amekuwa akiituhumu Paris na washirika wake kwa kupanga njama za kuisambaratisha Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES) kupitia mitandao ya siri, makundi yenye silaha, na wafuasi wa kikanda.