Mali: Wanajeshi 82 waliotekwa nyara na makundi yenye silaha wameachiliwa huru
-
Mali: Wanajeshi 82 waliotekwa nyara na makundi yenye silaha wameachiliwa huru
Serikali ya Mali imetangaza kuwa wanajeshi wake 82 waliokuwa wametekwa nyara na makundi yenye silaha wameachiliwa huru.
Taarifa ya jeshi la Mali imesema kuwa, wanajeshi hao walikuwa wamezuiliwa kama wafungwa na makundi ya Tuareg pamoja na makundi yenye silaha ambayo yana uhusiano na mtandao wa kigaiidi wa al-Qaeda katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika.
Jeshi la Mali lilitangaza kuachiliwa huru wanajeshi hao siku ya Alkhamisi kupitia taarifa iliyotangazwa na televisheni ya taifa. Jeshi hilo limesema kuwa wanajeshi walioachiliwa walikuwa “wakishikiliwa mateka” na wapiganaji wenye uhusiano na mtandao wa al-Qaeda pamoja na kundi la waasi wanaotaka kujitenga, tangu mashambulizi yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali nchini humo mwezi Aprili mwaka huu.
Taarifa hiyo ilisema: “Kuachiliwa kwao ni kilele cha mchakato ulioanzishwa mara moja baada ya kutekwa kwao,” na kuongeza kuwa wanajeshi hao wako salama na wako chini ya uangalizi wa mamlaka.
Kundi lenye uhusiano na mtandao wa al-Qaeda, Jama’at Nusrat al-Islam wal Muslimin (JNIM), pamoja na Azawad Liberation Front (FLA) inayoongozwa na Watouareg, yalidai kuhusika na mfululizo wa mashambulizi yaliyofanyika tarehe 25 Aprili, yakilenga uwanja wa ndege wa Bamako na maeneo mengine kadhaa.
Waziri wa Ulinzi wa Mali, Sadio Camara, aliuawa katika shambulio la bomu lililolenga makazi yake katika mji wa Kati.
Makundi hayo mawili pia yalidai kuhusika na mashambulizi dhidi ya vituo vya jeshi katika maeneo mbalimbali nchini Mali tarehe 4 Julai.
FLA ilisema katika taarifa yake siku ya Alhamisi kwamba, imewaachilia huru takribani wanajeshi 80 wa Mali waliokuwa wanashikiliwa mateka kati ya mwaka 2023 na 2026. Hata hivyo, kundi hilo halikutoa mara moja maelezo kuhusu tofauti hiyo na taarifa ya jeshi la Mali kwamba, wanajeshi hao walikuwa wamezuiliwa tangu mashambulizi ya tarehe 25 Aprili.
Mohamed Elmaouloud Ramadane, msemaji wa FLA, alisema kuachiliwa wanajeshi hao kulifanyika kwa “sababu za kibinadamu pekee.”