Milio ya risasi yasikika katika mji mkuu wa Niger, Niamey
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139240-milio_ya_risasi_yasikika_katika_mji_mkuu_wa_niger_niamey
Milio ya risasi imesikika mapema leo Alkhamisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Diori Hamani mjini Niamey, nchini Niger, miezi kadhaa baada ya shambulio kubwa la waasi katika eneo hilo hilo.
(last modified 2026-06-18T10:11:45+00:00 )
Jun 18, 2026 10:06 UTC
  • Milio ya risasi yasikika katika mji mkuu wa Niger, Niamey

Milio ya risasi imesikika mapema leo Alkhamisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Diori Hamani mjini Niamey, nchini Niger, miezi kadhaa baada ya shambulio kubwa la waasi katika eneo hilo hilo.

Mapema leo ripoti zilisema, eneo hilo la uwanja wa ndege lilizingirwa na kwamba washambuliaji wamefanikiwa kuingia katika uwanja wa ndege.

"Nilisikia milio ya risasi ya kwanza yapata saa kumi na mbili alfajiri. Milio ya risasi ilikuwa ikitokea kwenye lango la uwanja wa ndege na iliendelea saa mbili baadaye", amesema mkazi mmoja wa Niamey.

Mwezi Januari mwaka huu, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Diori Hamani mjini humo ulilengwa katika shambulio ambalo halijawahi kutokea lililodaiwa kufanywa na waasi wa Daesh katika eneo la Sahel (EIS) na baadaye lilizimwa na vikosi vya jeshi la Niger vikisaidiwa na wapiganaji Russia.

Kufuatia shambulio hilo, maelfu ya nyumba zilizokuwa zimejengwa kinyume cha sheria katika kitongoji kikubwa karibu na uwanja huo wa ndege zilibomolewa. Serikali ya Niger ilisema wilaya hiyo ilikuwa imeingiliwa na wapiganaji wa makundi ya waasi kwa ajili ya kutekeleza shambulio hilo.

Niger, nchi pana ya eneo la Sahel magharibi mwa Afrika, imekuwa ikipambana na hujuma za makundi yenye silaha yenye uhusiano na Al-Qaeda na kundi la daesh kwa muongo mmoja.