Maombolezo ya Imam Askari (AS) Hadi Mapambazuko ya Matumaini
-
Kuawa shahidi Imam Hassan Askari (AS)
Tarehe 8 na 9 za mwezi wa Rabiul al-Awwal ni siku mbili zinazofuatana katika kalenda ya Waislamu wa madhehebu ya Shia: Moja huwa ni siku ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hassan al-Askari (AS), na nyingine huashiria kuanza uongozi wa Imam wa Zama (AS).
Katika sehemu hii ya kipindi chetu, tunajadili maisha, changamoto, pamoja na urithi wa kielimu na kiroho wa Imam wa Kumi na Moja katika kizazi cha Mtume wetu Muhammad (SAW). Vilevile tunazungumzia kipindi cha kuanza ukurasa mpya katika historia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na zama za Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake); ukurasa ambao umeunganishwa kwa karibu sana na dhana ya "kungojea" pamoja na matumaini ya kudhihirika haki na uadilifu.
Tarehe 8 na 9 Mfunguo Sita Rabiul Awwal ni siku zenye umuhimu mkubwa na nafasi ya kipekee katika historia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia; ni siku ambazo kwa upande mmoja zinaashiria kumbukumbu ya kuuawa kikatili Imam Hassan al-Askari (AS)—Imam wa Kumi na Moja wa Waislamu wa madhehebu ya Shia; na kwa upande mwingine, mwanzo wa Uimamu wa Hadhrat Waliyyul-Asr (AS)—Huja wa mwisho ya Mungu na Mwokozi aliyeahidiwa wa Akheri Zamani au zama za mwisho za dunia. Matukio haya mawili si matukio ya kihistoria yaliyojitenga tu; bali ni viungo vilivyounganishwa katika mnyororo wa Uimamu na mwongozo wa watukufu— mnyororo ambao hauishii kwenye kuuliwa shahidi kwa Imam, bali huhakikisha kuwa jukumu la kuongoza na kuisimamia Umma linaendelea kupitia kwa Imam anayefuata.
Imam Hassan al Askari (AS) alizaliwa mwaka 232 Hijria mjini Madina. Mama yake alikuwa mwanamke mtukufu na mwenye fadhila ambaye alimlea mwanawe kwa uangalifu mkubwa, akihakikisha kuwa analelewa kwa namna inayostahili. Aliishi kwa muda wa miaka 29; miaka 13 ya kwanza ya maisha yake aliishi katika mji wa babu yake, Madina. Kipindi cha pili kilichoendelea kwa miaka 10 aliishi Samarra huko Iraq kabla ya kipindi chake cha Uimamu; na kipindi cha tatu kilijumuisha takriban miaka sita ya Uimamu wake.
Imam Hassan al-Askari (AS) alitumia miaka mitatu kati ya miaka sita ya Uimamu wake akiwa gerezani. Wakati alipokuwa gerezani, matendo na harakati zake zote zilifuatiliwa kwa uangalifu mkubwa, hata hivyo walinzi wawili waliopangiwa kumchunga kwa karibu- baada ya kushuhudia mienendo na tabia yake walivutiwa na mtukufu huyo na kuamiliana naye kwa wema.
Ubaydullah Khaqan, waziri mwaminifu wa utawala wa Bani Abbas, licha ya tabia yake ya kiburi na majivuno alikuwa akisimama kwa heshima kila alipokutana na Imam al-Askari (AS); akimkalisha Imam katika nafasi yake na mara kwa mara alikuwa akisema: "Sijawahi kuona mtu yeyote hapa Samarra kama mtukufu huyu; Ni mchamungu na mwenye elimu kubwa kuliko wote katika zama hizi."
Imam Hassan al Askari (AS) hakuwa shakhsia wa kisiasa au kiongozi wa kidini tu; bali pia alikuwa na nafasi muhimu katika nyanja za elimu, sayansi na maarifa ya dini. Walikuwa wakimuuliza maswali mbalimbali kuhusu Qur'ani, sheria za dini pamoja na masuala ya imani na maadili. Majibu ya Imam yamehifadhiwa katika mkusanyiko wa vyanzo vya Kiislamu. Mojawapo ya kazi muhimu zaidi za Maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume Muhammad (SAW) katika kipindi hicho ilikuwa kukabiliana na upotovu wa kifikra. Jamii ya Kiislamu ilikabiliwa na mirengo mbalimbali ya kiitikadi na kifikra, na ilikuwa wajibu wa Imam kubainisha mipaka ya imani na itikadi sahihi ya Kiislamu. Imam Hassan al Askari (AS) pia alifanya bidii kuwahimiza wafuasi wake kuwa na uelewa sahihi wa dini na kuzingatia uchamungu, ukweli, uaminifu na kuheshimu haki za wengine.
Imam Askari (AS) aliishi katika zama ambazo serikali ya Bani Abbas ilihofia sana ushawishi wa kiroho na kijamii wa Ahlul Bayt (AS). Lakabu maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni "Askari." Askar ni jina la eneo moja huko Samarra; na kwa kuwa Imam alilazimishwa kuishi huko kwa amri ya mtawala wa Bani Abbas alijulikana kwa jina la Askari. Lakabu nyingine ya Imam Hasan al Askari (AS) ni "al-Faqih". Hii inaonyesha kuwa Imam alikuwa maarufu miongoni mwa masahaba wake katika uga huo wa taaluma ya sheria za Kiislamu. Baadhi ya Hadithi zake zinahusiana na masuala ya fiqhi na minyambuliko yake. Mengi yamesemwa kuhusu umahiri wa kielimu wa Imam Hassan al Askari (AS). Ya'qub ibn Is'haq al-Kindi mwanafalsafa mashuhuri wa Kiarabu ambaye msomi maarufu wa Kiirani, Abu Nasr Farabi alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa shule yake, alipigwa na mshangao mkubwa wakati wa mjadala na Imam Askari, na baadaye akawa mmoja wa watu waliomkubali na kumfuata. MUZIKI
Mojawapo ya majukumu muhimu zaidi ya mtukufu huyo ilikuwa kuandaa wafuasi wake kwa ajili ya kipindi cha ghaiba ya Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake). Mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Imam na Mashia na wafuasi wake hayakuwezekana kutokana na vikwazo vya serikali; hivyo, hatua kwa hatua Mashia walijifunza jinsi ya kulinda mafundisho yao ya kidini katika mazingira magumu, jinsi ya kuwasiliana na Imam kupitia watu wa kati wanaoaminika, na jinsi ya kukabiliana na mirengo potofu pamoja na propaganda za utawala dhalimu wa Bani Abbas. Mmoja wa watu mashuhuri zaidi katika uwanja huu alikuwa Uthman ibn Sa'id ambaye baadaye alipata hadhi ya kipekee wakati wa kipindi cha ghaiba ya Imam Mahdi (AS). Mtandao huo wa mawasiliano ulikuwa na umuhimu mkubwa katika kipindi hicho ambapo Imam hakuwa na uwezo wa kukutana kwa uhuru na wafuasi wake. Katika mchakato huu, Imam Askari (AS) hakuwa kiongozi wa zama zake pekee; bali alikuwa akitayarisha jamii ya Waislamu kwa ajili ya kipindi cha baadaye ambapo Imam atatoweka mbele ya macho ya watu. Awamu hii ya historia ya Mashia na wafuasi wa Ahlul Bayt ilikuwa kipindi nyeti sana, kwani maadui wa Watu wa Nyumba ya Mtume (SAW) walikuwa wakijua vyema habari njema zilizotolewa na Mtume (SAW) pamoja na Maimamu Maasumu (AS) kuhusu kudhihiri Mwokozi wa Akheri Zamani; walijua kuwa Mahdi Aliyeahidiwa (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiriki kwake) angetoka katika kizazi cha Mtume Muhammad (SAW) na katika Ahlul-Bayt (AS). Kwa msingi huo, kuzaliwa na maisha ya Imam Mahdi (AS) vilitokea katika mazingira ya kipekee na viliambatana na tahadhari pamoja na uangalifu mkubwa sana.
Mwaka 260 Hijria, Samarra ilishuhudia mojawapo ya matukio ya kuhuzunisha zaidi katika historia ya Ahlul-Bayt (AS). Imam Hassan al-Askari (AS) aliuawa shahidi wakati utawala wa Bani Abbas ulikuwa ukifuatilia shughuli zake kwa hisia na wasiwasi mkubwa. Vyanzo vya historia vinasema aliuawa shahidi tarehe 8 Rabiul Awwal. Imamu huyo ambaye alitumia sehemu kubwa ya kipindi chake cha uimamu katika mazingira ya ukandamizaji na ufuatiliaji mkali wa utawala wa Bani Abbas, hatimaye aliuawa shahidi akiwa bado kijana. Hata hivyo, urithi aliouacha ulikuwa mfano wa kudumu wa subira, kujitolea, elimu, Uchamungu, uwajibikaji na msimamo thabiti dhidi ya dhuluma na ukandamizaji.
Historia inaonyesha kuwa Maimamu katika kizazi cha Mtume (SAW) hawakuwa chini ya mashinikizo ya tawala zilizokuwa madarakani kwa sababu tu ya ibada zao au maisha yao binafsi; bali, uwepo wao ulikuwa tishio kubwa kwa tawala za kidhalimu. Waliwalingania watu kuzingatia utu, haki, uhuru na imani ya Mungu Mmoja, wito uliotikisa misingi ya tawala za kidikteta. Kuuliwa shahidi Imam Hassan al Askari pia kulitokana na hofu na wasiwasi uliochochewa na Hadithi za kuaminika zilizomfikia mtawala Mu'tasim al-Abbasi pamoja na makhalifa waliomtangulia na wa baada yake; ambazo zilitabiri kuwa mtoto mwenye nasaba tukufu, atakayepewa jina la Mtume Muhammad (SAW) na kufahamika kama "Mahdi wa Zama za Mwisho," angezaliwa na Nargis Khatun na Imam Hassan al Askari (AS), na kwamba angeangusha viti vya enzi vya madhalimu na kuhitimisha utawala na mamlaka yao.
Inaaminika kuwa Imam Askari (AS) aliuliwa shahidi kwa sumu aliyowekewa kwenye chakula na Mu'tamid al-Abbasi. Baada ya Waislamu kupata habari ya kuuliwa shahidi Imam Hassan Askari (AS), wingu la majonzi na huzuni lilitanda juu ya mji wa Samarra; sauti za vilio na maombolezo zilisikika kutoka kila pembe, huku watu wakijiandaa kuomboleza na kuandaa ya mazishi ya mtukufu huyo.
Ingawa kuuawa shahidi Imam Hassan Askari (AS) ulikuwa msiba mkubwa kwa Waislamu hasa wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume, lakini haukuwa mwisho wa njia ya Uimamu. Katika mantiki ya teolojia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, dunia haiwezi kubakia bila ya kuwepo hujja wa Mungu, na anapouliwa shahidi imam, jukumu la kuongoza Umma huhamia kwa Imam anayefuata. Kwa mtazamo huu, kuuawa shahidi Imam wa Kumi na Moja kunapasa kutambuliwa kuwa ni hatua ya kihistoria ya kuhamia jukumu ya Uimamu kwa Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake). Kwa msingi huo, siku ya tisa ya mwezi wa Rabiul Awwal huadhimishwa katika utamaduni wa Waislamu wa madhehebu ya Shia kama mwanzo wa Uimamu wa Imam wa Zama, Mahdi (Mwenyezi Mungu na aharakishe kudhihiri kwake).
Katika upande mwingine, uimamu wa Mtukufu Mahdi (AS) unaangazia maana ya "kungojea" katika maisha ya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Katika utamaduni wa Mahdism, "kungojea" hakumaanishi kukaa tu bila kufanya lolote ukisubiri kubadilika hali ya mambo; bali, kungojea halisi ni hali ya utayarifu wa kudumu wa kufuata haki na uadilifu. Mtu anayesubiri kudhihiri Imam wa Zama ni yule anayejirekebisha, anayeacha uongo na ukandamizaji, anayeheshimu haki za watu wengine, anayepambana na ufisadi, na anayejitahidi kujenga jamii yenye maadili na haki.. Ikiwa jamii inatarajia haki ya kimataifa, ni lazima kwanza ianzie kwake yenyewe na kujirekebisha kutokea ndani. Mtu yeyote anayewadhulumu wanadamu wengine katika maisha yake binafsi, bado hajafahamu maana halisi ya *Entezar* (au kungojea kudhihiri Imam wa Zama). Entezar ya kweli humfanya mtu kuwajibika zaidi, kuwa mwadilifu zaidi, mwenye matumaini zaidi, na mwenye maadili mema zaidi.
Kuhamishwa Uimamu kutoka kwa Imam Hassan Askari (AS) kwenda kwa Imam Mahdi (AS) kimsingi ni makabidhiano ya jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu kutoka kizazi kimoja hadi kingine na kukabidhiana bendera ya harakati za kupigania haki, na mapambano dhidi ya dhulma na ukandamizaji. Kwa hiyo, hakuna pengo linalopaswa kuwepo kati ya "kuuawa shahidi" Imam Hassan Askari na "Kuanza Uimamu" wa Imam wa Zama. Kidhahiri, tarehe 8 Rabiul Awwal inaashiria kuuliwa shahidi Imam, na tarehe 9 ya Rabiul Awwal inakumbusha kuendelezwa njia ya Uimamu. Siku hizi mbili, zinapoadhimishwa pamoja zinatoa ujumbe wa wazi: Njia ya kupigania haki na kweli haisimami kutokana na kuuawa shahidi viongozi walioteuliwa na Mungu.
Asanteni kwa kuwa nasi na kwaherini.....