Jumamosi, 22 Agosti 2026
-
Leo katika Historia
Leo ni Jumamosi 9 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1448 Hijria mwafaka na 22 Agosti 2026 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1188 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, baada ya kuuawa shahidi Imam Hassan Askari (AS), kilianza rasmi kipindi cha uongozi wa Imam wa Zama, Imam Mahdi (AF). Imam Mahdi ni mwana wa Imam Hassan al Askari (AS) na miongoni mwa wajukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw). Imam Mahdi yuko ghaiba kwa amri ya Mwenyezi Mungu (SW) na hadi mwaka 328 Hijria alikuwa akiwasiliana na watu kupitia wawakilishi wake maalumu. Kipindi hicho kilipewa jina la "Ghaiba Ndogo". Baada ya hapo kilianza kipindi cha Ghaiba Kubwa ambapo Imam wa Zama hakuainisha mwakilishi makhsusi, na mafaqihi wenye ujuzi wa dini ya Kiislamu, wachamungu na watambuzi wa masuala ya zama ndio wawakilishi wa mtukufu huyo katika Umma. Kwa mujibu wa Hadithi tukufu za Mtume Muhammad (saw), Imam Mahdi (AF) atadhihiri tena katikka aheri zamani kwa ajili ya kueneza haki na uadilifu.
Katika siku kama ya leo miaka 399 iliyopita, vita vya mwisho vya La Rochelle kati ya Wakatoliki na Waprotestanti nchini Ufaransa vilianza. Vita hivyo vilichochewa na Uingereza, ambayo iliwahamasisha Waprotestanti wa Ufaransa kuupinga utawala wa Wakatoliki. Wakatoliki, wakisaidiwa na vikosi vya serikali ya Ufaransa vilivyoongozwa na Kadinali Richelieu, ambaye alikuwa Kansela maarufu wa nchi hiyo, walianza kupambana na Waprotestanti waliokuwa wakilinda ngome zao katika bandari ya La Rochelle, iliyoko magharibi mwa Ufaransa. Baada ya takribani mwaka mmoja wa mapigano, vita hivyo vilimalizika kwa ushindi wa Wakatoliki na kutekwa kwa mji wa La Rochelle.
Siku kama ya leo miaka 328 iliyopita, muungano wa pande tatu kati ya Urusi, Poland na Denmark dhidi ya Sweden ulitiwa saini. Wafalme wa nchi hizo tatu walikusudia kumshinda Mfalme Karl XII, mfalme kijana wa Sweden, na kisha kuiteka nchi hiyo. Kwa msingi huo, miaka miwili baadaye, mwezi Aprili 1700, nchi zilizokuwa wanachama wa muungano huo ziliishambulia Sweden. Hata hivyo, jeshi la Mfalme Karl XII lilipambana kwa ujasiri dhidi ya wavamizi na kuwashinda. Baada ya kufanya amani na Denmark, Karl XII aliishambulia Poland mwaka 1704 na kuiteka nchi hiyo. Hata hivyo, uvamizi wake dhidi ya Urusi haukufanikiwa.
Miaka 208 iliyopita, tarehe 22 Agosti 1818: Warren Hastings, mwanasiasa wa Kiingereza na Gavana Mkuu wa kwanza wa kikoloni wa Uingereza nchini India, alifariki dunia. Hastings alizaliwa mwaka 1732. Akiwa kijana, alianza kufanya kazi kama karani katika Kampuni ya Kiingereza ya India Mashariki. Taratibu alipanda katika vyeo mbalimbali hadi mwaka 1768, alipokabidhiwa uongozi wa Jimbo la Bengal nchini India. Miaka sita baadaye, mwaka 1774, aliteuliwa kuwa Gavana Mkuu wa kwanza wa Uingereza nchini India, nafasi aliyoishikilia hadi mwaka 1784, kwa kipindi cha miaka kumi. Ingawa Uingereza ilifanya uhalifu na ukatili mwingi nchini India, miaka ya utawala wa Hastings inatajwa kuwa miongoni mwa vipindi vya giza zaidi katika historia ya ukoloni wa Uingereza nchini humo. Alipanua maeneo yaliyotekwa na kukaliwa na Uingereza nchini India, akawashinikiza wananchi kwa mbinu kali sana, na kuyakandamiza kwa ukatili mkubwa maasi dhidi ya utawala wake. Aidha, alihusika katika matukio mengi ya ufisadi wa kifedha. Hatimaye, baadhi ya wanafikra na wapinzani wake wa kisiasa walimshinikiza Hastings na kumfikisha mahakamani ili ajibu tuhuma zilizokuwa dhidi yake. Hata hivyo, hakupatikana na hatia, na badala yake, baadaye aliheshimiwa na kusifiwa.
Siku kama ya leo miaka 166 iliyopita Paul Gottlieb Nipkow mmoja wa wavumbuzi wa televisheni alizaliwa huko Ujerumani. Nipkow alikulia katika familia maskini, lakini juhudi na irada kubwa ilimuwezesha kuendeleza masomo yake ya fizikia hadi chuo kikuu. Paul Gottlieb Nipkow alifanya utafiti mkubwa na hatimaye alifanikiwa kuvumbua transimita ya televisheni. Chombo hicho kilichobuniwa na Nipkow kiliweza kurusha mawimbi ya televisheni katika umbali wa mita 30 na baadaye transimita iliyotengenezwa na mvumbuzi huyo wa Kijerumani ilikamilishwa na wabunifu wengine.
Na miaka 162 iliyopita katika siku kama hiii ya leo, mkataba wa kihistoria wa Geneva ulitiwa saini baina ya nchi kadhaa za Ulaya, Asia na Amerika. Lengo la mkataba huo lilikuwa ni kuwasaidia majeruhi katika medani za vita. Kwa mujibu wa mkataba huo, timu za madaktari, watoaji misaada na zana zao zinapaswa kutoegemea upande wowote na zisishambuliwe bali zibakie katika amani wakati wa vita. Mbunifu wa mkataba huo alikuwa Henry Dunant raia wa Uswisi.