WFP: Mamilioni ya watu wanakabiliwa na baa la njaa nchini Somalia
-
Somalia na baa la njaa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa, watu milioni sita nchini Somalia wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa WFP, Carl Skau, amesema shirika hilo sasa lina rasilimali mara kumi pungufu ukilinganisha na mwaka 2022, wakati liliposaidia kuzuia kutokea kwa njaa kubwa nchini Somalia.
Skau amesema ukosefu wa fedha, kutokana na kupunguzwa misaada ya kimataifa na kuelekezwa kwa migogoro mingine, umeifanya WFP kushindwa kuongeza msaada wake.
Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, takriban watu milioni 6.5 wanakabiliwa na njaa kali kutokana na ukame ulioikumba Somalia.
Mwaka huu, watoto milioni 1.9 walio chini ya miaka mitano wanatarajiwa kukabiliwa na utapiamlo mkali, huku karibu nusu milioni wakihitaji matibabu ya haraka.
Katika kituo cha afya cha Feynuus mjini Mogadishu, mamia ya wanawake na watoto waliohamishwa kutoka maeneo mengine hufika kila siku kutafuta msaada. Kituo hicho hupokea wagonjwa kati ya 250 na 350 kwa siku.
Kituo hicho sasa kinakabiliwa na msongamano mkubwa baada ya takribani vituo kumi vya afya na lishe kufungwa kutokana na kupungua kwa ufadhili na misaada.
WFP inasema ukame, migogoro, watu kuyahama makazi yao na kupanda bei za chakula vimeongeza hali hiyo. Shirika hilo linaonya kuwa bila rasilimali zaidi, mamilioni ya Wasomali wanaweza kukosa msaada wanaouhitaji kwa haraka.
Katika ripoti yake ya hivi karibuni ya kibinadamu, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema kuwa misururu ya migogoro, ikiwemo ukame mkali, mafuriko, kupungua kwa misaada, na mzozo wa muda mrefu, imeendelea kudhoofisha kwa utaratibu uwezo wa mamilioni ya familia za Kisomali kustahimili hali hiyo.