Mahakama ya Tanzania: Tundu Lissu ana kesi ya kujibu ya uhaini
-
Tundu Lissu, Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania
Mahakama Kuu ya Tanzania imeamua kwamba Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, Tundu Lissu, ana kesi ya kujibu katika kesi ya uhaini inayomkabili, hatua inayofungua njia kwa mwanasiasa huyo kuanza kujitetea.
Uamuzi huo umetolewa le Ijumaa, Agosti 21, 2026, na Jaji Dunstan Ndunguru, anayeongoza jopo la majaji watatu. Majaji wengine ni James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
"Mahakama imeamua kwamba upande wa mashtaka umejenga kesi ambayo mshtakiwa anapaswa kuijibu,” amesema Jaji Ndunguru.
Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kuchunguza ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka pamoja na hoja za Lissu, ambaye aliiomba iachilie mbali kesi hiyo kwa madai kwamba hakuna ushahidi wa msingi unaomhusisha na kosa la uhaini.
Uamuzi huo haumaanishi kwamba Lissu amepatikana na hatia. Unamaanisha kwamba mahakama imeona kuna ushahidi wa awali unaohitaji majibu kutoka kwa mshtakiwa kabla ya uamuzi wa mwisho kutolewa.
Jaji Ndunguru amesema jukumu la mahakama katika hatua hiyo lilikuwa kuamua ikiwa ushahidi wa upande wa mashtaka, endapo hautapingwa, unaweza kutosha kumtia mshtakiwa hatiani.
Mahakama haikuhitajika kufanya uchambuzi wa kina kuhusu uzito au uaminifu wa kila ushahidi katika hatua hii. Masuala hayo yatazingatiwa baada ya Lissu kuwasilisha utetezi wake.
Kwa mujibu wa mahakama, ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka ulimhusisha Lissu kwa kiwango kinachotosha na matamshi yaliyowekwa katika hati ya shtaka.
Upande wa mashtaka uliita mashahidi 17 kati ya 30 waliokuwa wameorodheshwa kabla ya kufunga ushahidi wake Agosti 17. Waendesha mashtaka waliiambia mahakama kwamba ushahidi huo ulitosha kuthibitisha hoja muhimu za shtaka na kumtaka Lissu ajitetee. Kwa upande wake Lissu, anayejitetea mwenyewe, aliiomba mahakama imwachilie huru akisema upande wa mashtaka haukuonyesha kitendo chochote kinachoweza kutafsiriwa kuwa uhaini.