Namna shambulio la kijeshi dhidi ya Iran lilivyoikatisha tamaa Ulaya
Vita vinavyoendeshwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran si mgogoro wa kijeshi wa eneo dogo tu katika Asia Magharibi. Kufungwa Lango-Bahari la Hormuz na kuvurugika kimataifa usambazaji wa nishati kumetikisa uchumi wa dunia nzima, ambapo madhara yake yanaonekana wazi hadi katika kitovu cha Ulaya na Uingereza.
Kwa upande wa Ulaya, suala hili linavuka mipaka ya kupanda kwa bei ya mafuta na gesi tu ambapo athari za vita sasa zimeenea hadi kwenye mifumuko ya bei, viwango vya riba, uwekezaji, uzalishaji, madeni ya serikali na hatimaye siasa za ndani za nchi za bara Ulaya. Lango-Bahari la Hormuz ni mojawapo ya maeneo muhimu zaidi ya usambazaji nishati duniani. Usumbufu katika njia hii, hata kama hautasimamisha moja kwa moja mauzo ya nishati barani Ulaya, lakini bila shaka unaongeza bei za mafuta, gesi, bidhaa za petroli na usafirishaji duniani. Katika ripoti yake ya Julai, Benki ya Uingereza ilielezea mgogoro katika Asia Magharibi na usumbufu katika Lango-Bahari la Hormuz kama "mshtuko hasi wa usambazaji" kwa uchumi wa dunia. Benki hiyo ilionya kwamba mshtuko endelevu wa nishati unaweza kuchochea mfumuko wa bei nchini Uingereza na kuongeza mashinikizo kwa raia na biashara.
Uingereza inakabiliwa na hali ngumu sana katika uwanja huo ambapo uchumi wake bado unakabiliwa na ukuaji mdogo, gharama kubwa za kukopa na mashinikizo kwenye fedha za umma. Benki ya Uingereza iliainisha kiwango chake cha riba kuwa 3.75% mwezi Julai, ingawa wajumbe watatu wa Kamati ya Sera za Fedha walipendekeza kuongezwa kiwango hicho hadi 4%. Benki hiyo imebainisha kuwa kupanda kwa bei za nishati kunaweza kuchochea mfumuko wa bei unaoendelea na hatimaye kuathiri vibaya gharama za uzalishaji, usafirishaji na mishahara.
Gharama kubwa za nishati huongeza gharama za uzalishaji, ambazo nazo huchochea mfumuko wa bei ya mafuta; mfumuko wa bei unaosababisha viwango vya juu vya riba, na viwango vya juu vya riba husababisha kupungua kwa matumizi. Makampuni madogo na ya kati ndiyo huwa ya kwanza kuathirika katika hali kama hiyo. Onyo la kampuni ya "Azets" kuhusu mashinikizo yanayoongezeka katika sekta za viwanda, usafirishaji wa bidhaa (logistics), uchukuzi, huduma za hoteli na ujenzi linaonyesha kuwa mzozo huo umehamia kutoka masoko ya fedha hadi kwenye uchumi halisi.
Katika muktadha huu, mabadiliko ya uongozi mjini London yana umuhimu wa kipekee. Andy Burnham amekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza tangu tarehe 20 Julai mwaka huu. Yeye ni Waziri Mkuu wa saba wa nchi hiyo tangu mwaka 2016 na mtu wa sita kuingia Downing Street ndani ya muongo mmoja. Burnham aliingia madarakani akiwa na ajenda ya kuleta uthabiti, ufufuaji wa uchumi na ugatuzi wa madaraka kutoka Westminster kwenda maeneo ya ndani ya nchi. Aliahidi kuwa serikali itashughulikia zaidi masuala ya huduma za umma, nishati, makazi, na miundombinu, na kwamba mifumo ya umma itatumika kwa ajili ya kujenga upya uwezo wa viwanda wa Uingereza. Hata hivyo, vita dhidi ya Iran sasa vinaathiri moja kwa moja utekelezaji wa ahadi hizo zinazotegemea pakubwa rasilimali za kifedha za serikali.
Serikali ya Burnham haiwezi kudhibiti kwa wakati mmoja gharama za nishati kwa familia, kusaidia biashara zilizo katika mazingira magumu, kupanua huduma za umma, kuongeza uwekezaji katika miundombinu, na wakati huo huo kudhibiti deni la taifa. Burnham mwenyewe amekuwa akisisitiza kuwa serikali inakabiliwa na hali ngumu kifedha. Hivyo, mgogoro katika Lango-Bahari la Hormuz si mgogoro wa kiuchumi tu kwa Burnham bali ni mtihani wa kisiasa. Iwapo gharama za nishati na bei za bidhaa zitapanda, uungwaji mkono wa umma kwa serikali yake utapungua. Iwapo viwango vya riba vitaendelea kuwa juu au kupanda, mashinikizo ya mikopo ya nyumba, biashara, na uwekezaji yataongezeka. Iwapo serikali itaongeza kodi au kuongeza deni ili kukabiliana na mashinikizo hayo, itakabiliwa na upinzani wa kisiasa.
Nchi nyingine za Ulaya zinajikuta katika hali kama hiyo. Mashambulio zaidi ya kijeshi yanayoweza kufanywa na Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Iran bila shaka yatazidisha mgawanyiko kati ya sera za kigeni za serikali za Ulaya na maslahi ya kiuchumi ya raia wao. Ingawa serikali za Ulaya zinaweza kuzungumzia usalama wa nishati na ushirikiano wao na Marekani, raia wa kawaida wa Ulaya huhisi gharama za sera hizo kupitia bili za umeme, bei za mafuta na chakula, pamoja na viwango vya riba ya mikopo. Hapa ndipo madhara ya kisiasa ya vita yanapojitokeza wazi. Mgogoro wa nishati unaweza kuimarisha vyama vya upinzani, makundi ya mrengo wa kulia na harakati zinazopinga utegemezi wa usalama wa Ulaya kwa Washington. Kadiri vita vinavyoendelea kwa muda mrefu, ndivyo maoni ya umma yanavyozidi kubadilika: Kwa nini Ulaya ibebe gharama za kiuchumi za vita vilivyoanzishwa na kuendelezwa kutokana na maamuzi yaliyofanywa Washington na Tel Aviv?
Mgogoro wa nishati uliofuatia vita vya Ukraine ulionyesha wazi jinsi Ulaya ilivyo katika hatari ya kuathiriwa na misukosuko ya kijiopolitiki. Sasa, Lango-Bahari la Hormuz limedhihirisha tena udhaifu huo. Tofauti ya tukio la sasa ni kwamba mgogoro huo unahusiana moja kwa moja na suala la uhuru wa kimkakati wa Ulaya. Ulaya haiwezi kukabidhi usalama wake mikononi mwa Marekani na wakati huo huo kutarajia kuepuka kulipa gharama za kiuchumi zinazotokana na maamuzi ya usalama ya Washington. Mgogoro wa Lango-Bahari la Hormuz limeweka wazi zaidi ukweli huo. Vita dhidi ya Iran vinaweza kuvuruga utulivu wa kiuchumi na kisiasa wa Ulaya kwa muda mrefu kabla ya kuwa tishio la moja kwa moja la kijeshi. Ikiwa mgogoro utaendelea, uwanja wa vita utahama kutoka Lango-Bahari la Hormuz hadi viwanda, masoko ya nishati, bajeti za serikali na masanduku ya kupigia kura. Burnham aliwasili karibuni katika Mtaa wa Downing, lakini mtahani wake wa kwanza mkubwa unahusiana na matukio ambayo yako nje ya udhibiti wa London. Huenda huu ukawa ujumbe muhimu zaidi wa kisiasa wa mgogoro uliopo: Ulaya sasa inalipa gharama kubwa zaidi kuliko hapo awali, ya vita ambavyo inasema haikuwa na nafasi yoyote katika kuvianzisha wala kuwa na suluhisho la kuvimaliza.