Aug 20, 2026 02:58 UTC
  • Leo katika historia
    Leo katika historia

Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1448 Hijria, mwafaka na tarehe 20 Agosti 2026.

Katika siku kama ya leo miaka 1106 iliyopita Ali bin Muhammad Tanukhi alimu, mwandishi na malenga mashuhuri wa karne ya nne Hijria aliaga dunia katika mji wa Basra, kusini mwa Iraq akiwa na umri wa miaka 64.

Ali Tanukhi alizaliwa huko Antakia mashariki mwa Uturuki ya leo na akiwa kijana alielekea Baghdad na kuasisi makazi yake. Ali bin Muhammad Tanukhi alikuwa mahiri katika lugha na fasihi ya Kiarabu na kuwa miongoni mwa malenga mashuhuri wa zama hizo.

Mbali na kutunga diwani yake ya mashairi ambayo imebaki kama kumbukumbu hadi hii leo, Tanukhi ameandika pia vitabu mbalimbali kimojawapo kikiwa ni kile alichokipa jina la al Arudh.   ***

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels ulidhibitiwa na vikosi vya majeshi ya Ujerumani.

Huu ulikuwa mji mkuu wa kwanza kukaliwa kwa mabavu na Ujerumani wakati wa kujiriٰ Vita vya Kwanza vya Dunia.    ****

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita Marekani ilikiri kwamba ilifanya makosa kuishambulia ndege ya abiria ya Iran hapo tarehe 3 Julai mwaka 1988.

Siku hiyo ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege ya Iran iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas kusini mwa Iran na kuelekea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ilishambuliwa kwa makombora mawili kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani, USS Vincennes, ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu 298 waliokuwemo.

Shambulio hilo lilionyesha wazi unyama wa serikali ya Marekani na ukatili wake hata kwa wanawake na watoto wadogo waliokuwemo ndani ya ndege hiyo.

Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho kilichoonekana na serikali ya Washington kuwa eti ni cha kishujaa. ***  

Miaka 35 iliyopita, katika siku kama hii ya leo Estonia ambayo ni miongoni mwa nchi za Baltic huko magharibi mwa Urusi ya zamani, ilijitangazia uhuru.

Estonia ilikuwa chini ya satwa ya Urusi ya zamani kufuatia makubaliano ya siri yaliyofikiwa mwaka 1939 kati ya Hitler na Stalin. Mwaka 1991, karibu asilimia 80 ya wananchi wa Estonia walishiriki kwenye kura ya maoni na kupelekea kutangazwa uhuru wa nchi hiyo katika siku kama hii.

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, aliaga dunia Muhammad Hussein Behjati, mshairi na mwanazuoni mahiri wa Kiirani.

Alizaliwa 1314 Hijria Shamsia. Muhammad Hussein Behjati alianza kujihusisha na masomo tangu akiwa na umri wa miaka 7. Mwaka 1331 alielekea katika mji wa Qum.

Msomi huyo alisoma pamoja na shakshia mashuhuri kama Ayatullah Hashemi Rafsanjani, Mas'ud Khomeini na Ayatullah Ali Khamenei. Alikuwa pia mmoja wa wanafunzi wa Imam Khomeini na Ayatullah Burujerdi.