Ripoti: Vita vikishtadi, yamkini Iran ikavishambulia vituo vya Marekani barani Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140832-ripoti_vita_vikishtadi_yamkini_iran_ikavishambulia_vituo_vya_marekani_barani_ulaya
Gazeti la Financial Times limeripoti kuwa Iran inafikiria kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani barani Ulaya ikiwa Rais wa Marekani Donald Trump atashadidisha vita, wakati Tehran inazingatia pia machaguo ya kupanua wigo wa mzozo hadi nje ya Mashariki ya Kati.
(last modified 2026-08-20T11:54:52+00:00 )
Aug 20, 2026 11:46 UTC
  • Ripoti: Vita vikishtadi, yamkini Iran ikavishambulia vituo vya Marekani barani Ulaya

Gazeti la Financial Times limeripoti kuwa Iran inafikiria kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani barani Ulaya ikiwa Rais wa Marekani Donald Trump atashadidisha vita, wakati Tehran inazingatia pia machaguo ya kupanua wigo wa mzozo hadi nje ya Mashariki ya Kati.

Likiwanukuu watu wawili walio karibu na serikali ya Iran, gazeti hilo la kila siku la Uingereza limesema, vikosi vya Iran vimetathmini uwezekano wa kushambulia milki na vituo vya Marekani katika nchi za kusini mashariki mwa Ulaya, ikiwa ni pamoja na Bulgaria, ambayo mwezi uliopita iliidhinisha kutumiwa kambi yake ya anga ya Bezmer na ndege za Marekani za kujazia mafuta.

Kwa mujibu wa moja ya vyanzo hivyo viwili, Cyprus, ambayo ina kambi ya anga ya Uingereza iliyoshambuliwa na ndege isiyo na rubani mnamo mwezi Machi, nayo pia inafikiriwa kuwa miongoni mwa maeneo yanayoweza kulengwa endapo Marekani itaanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran.

Ripoti ya Financial Times imedai pia kuwa, vikosi vya Iran vimechunguza uwezekano wa kulenga nyaya za 'fiber-optic' za chini ya bahari katika Mlango Bahari wa Hormuz iwapo vita dhidi yake vitashadidishwa.

Chanzo kimoja kimeliambia gazeti hilo kwamba Tehran inaandaa machaguo ya kupanua mzozo endapo Trump atafuatilia kutekeleza vitisho alivyotoa awali vya kushambulia miundombinu ya Iran.

"Ikiwa Marekani itavuka kiwango, Iran itajihami kwa gharama yoyote, itavuka eneo na kuishambulia Ulaya pia," kimeeleza chanzo hicho.

 

Ripoti hiyo inatolewa wakati mazungumzo kuhusu kuufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz yakiwa yangali yamekwama huku matarajio ya kufanyika mazungumzo mapya kati ya Tehran na Washington yakiwa yamefifia.

Trump alitangaza siku ya Jumanne kuwa hakuna "mazungumzo au mazungumzo yanayoendelea, au yaliyopangwa (kufanyika)" na Tehran.

Mapema kabla ya hapo, maafisa wa kijeshi wa Iran walikuwa wameshaonya kwamba kituo chochote cha kijeshi kitachotumika kuanzishia mashambulizi dhidi ya ardhi ya Iran kitahesabiwa kuwa shabaha ya kushambuliwa.

Ripoti ya gazeti la Financial Times imewanukuu wataalamu wa kijeshi wakisema, Iran ina makombora yenye uwezo wa kufikia sehemu za kusini na kusini-mashariki mwa Ulaya, ingawa ufanisi na usahihi wake unaweza kupungua katika masafa marefu…/