May 12, 2020 21:50 UTC
  • Jumatano, 13 Mei, 2020

Leo ni Jumatano tarehe 19 Ramadhani 1441 Hijria, mwafaka na tarehe 13 Mei 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1401 iliyopita mwaka 40 Hijria Qamaria, Imam Ali bin Abi Talib AS ambaye ni mkwe, binamu na shakhsia wa karibu kwa Mtume Mtukufu SAW, alipigwa upanga wa sumu na kujeruhiwa vibaya akiwa anaswali swala ya alfajiri katika msikiti wa mji wa Kufa na mtu aliyeitwa Abdur Rahman bin Muljim Muradi. Imam Ali A.S alikufa shahidi baada ya siku 3. Ali bin Abi Talib ni shakhsia wa pili baada ya Mtume Mtukufu Muhammad SAW ambaye anaelezwa na historia ya Uislamu kuwa shujaa, mwenye imani, akhlaki njema, elimu na uadilifu. Alipata elimu na mafunzo kutoka kwa Mtume Mtukufu mwenyewe SAW, na alikuwa mwanamume wa kwanza baada ya Mtume SAW kuukubali Uislamu. Katika vipindi tofauti daima Imam Ali AS alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume SAW katika hali zote za shida na matatizo na hata kuhatarisha maisha yake ili kumlinda Mtume Mtukufu na dini ya Uislamu huku akionyesha ushujaa mkubwa katika vita mbalimbali vya haki dhidi ya batili. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji mashuhuri, Imam Ali AS alikuwa mpole na mwenye upendo. Kiasi kwamba moyo wake ulikuwa ni wenye kuathirika sana na kujawa na huruma alipoona machozi ya mtoto yatima. Imam Ali AS alipenda haki na uadilifu na kupambana vilivyo na dhulma katika kila njanya. Katika sehemu ya matamshi yake yenye hekima Imam Ali AS anasema: 'Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hata kama watanilaza bila ya nguo juu ya miiba ya jangwani, au kunifunga pingu na kamba na kuniburuza juu ya ardhi, kwangu mimi jambo hilo ni bora kuliko kukutana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake siku ya Kiama hali ya kuwa nimewadhulumu waja wake.'

Siku kama ya leo miaka 609 iliyopita alifariki dunia Ghiyathud-Din Jamshid Kashani, mwanahisabati na mtaalamu mashuhuri wa nyota wa Iran. Jamshid Kashani alikuwa mtaalamu mkubwa wa hesabati na mnajimu kama ambavyo alihusika katika kuvumbua vifaa vingi na zana muhimu za kufuatilia nyota. Aidha Ghiyathud-Din Jamshid Kashani alihusika katika ujenzi wa kituo cha kufuatilia harakati za nyota cha Samarqand. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameacha athari zenye thamani katika uga wa hisabati na nyota vikiwemo vitabu vya ‘Miftaahul-Hisaab’ na ‘Risaalatu Aalaat Rasad.’

Ghiyathud-Din Jamshid Kashani.

Siku kama ya leo miaka 307 iliyopita, sawa na tarehe 13 Mei 1713 Miladia, alizaliwa mjini Paris Alexis Cloude Clairaut mwanahesabati mashuhuri wa Ufaransa. Alikuwa na hamu kubwa na somo la hesabati ambapo akiwa na umri mdogo wa miaka 18 alifanikiwa kujiunga na Chuo cha Sayansi cha Ufaransa. Clairaut alipata umashuhuri mkubwa duniani kutokana na utafiti makini aliofanya katika nyanya tofauti za sayansi. Msomi huyo aliaga dunia mwaka 1765.

Alexis Cloude Clairaut

Siku kama ya leo miaka 267 iliyopita, sawa na tarehe 13 Mei 1753 Miladia, alizaliwa Lazar Carnot, mwanasiasa, jenerali na mtaalamu wa hisabati wa nchini Ufaransa. Msomi huyo anayehesabika kuwa mmoja wa waasisi wa elimu mpya ya uhandisi, alitabahari pia katika fani ya uhandisi na stratijia ya kijeshi huku akiwa mmoja wa viongozi wenye taathira katika ushindi tofauti wa wanamapinduzi wa nchi hiyo. Ni kwa ajili hiyo ndio maana akaitwa kwa lakabu ya 'roho ya kijeshi ya mapinduzi ya Ufaransa.' Baada ya ushindi wa mapinduzi ya nchi hiyo alishikilia nyadhifa mbalimbali za uongozi ikiwemo nafasi ya uanachama wa mkutano mkuu wa chama tawala na Wizara ya Vita ya Ufaransa. Lazar Carnot alifariki dunia mwaka 1823 Miladia.

Lazar Carnot

Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita, sawa na tarehe 13 Mei 1907 Miladia, alizaliwa Bi Daphne du Maurier mwandishi wa riwaya, wasifu na tamthiliya wa Uingereza. Maurier alizaliwa katika familia ya wasanii na iliyokuwa pia na wataalamu wa fasihi. Ni kutokana na kukulia katika mazingira hayo, ndipo Bi Daphne du Maurier akafanikiwa kukuza kipaji chake katika uwanja wa uandishi. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni Scapegoat na Rebecca. Mwandishi huyo aliaga dunia mwaka 1889.

Bi Daphne du Maurier

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita yaani sawa na tarehe 24 Ordebehesht 1363 Hijiria Shamsia, alifariki dunia mtafiti, mshairi na mwandishi wa Kiirani Habib Yaghmai. Alizaliwa mwaka 1280 Hijiria Shamsia. Mwishoni mwa masomo yake alijihusisha sana na kutalii na utafiti katika fani ya fasihi ya lugha ya Kifarsi na maarifa ya Kiislamu. Yaghmai alisahihisha tarjumi ya Twabari na athari za mashairi ya Saa'di.

Habib Yaghmai