Katibu Mkuu wa UN: Mkataba kuhusu wakimbizi si wa kupuuzwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i140244-katibu_mkuu_wa_un_mkataba_kuhusu_wakimbizi_si_wa_kupuuzwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa nchi zote wanachama kuhuisha dhamira yao ya kutekeleza Mkataba wa Wakimbizi wa mwaka 1951, akisema haki ya watu wanaokimbia mateso kutafuta hifadhi inazidi kutiliwa shaka, kuwekewa vikwazo au kunyimwa.
(last modified 2026-07-29T02:28:45+00:00 )
Jul 29, 2026 02:25 UTC
  • Guterres atilia mkazo kuhusu mkataba wa wakimbizi
    Guterres atilia mkazo kuhusu mkataba wa wakimbizi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa nchi zote wanachama kuhuisha dhamira yao ya kutekeleza Mkataba wa Wakimbizi wa mwaka 1951, akisema haki ya watu wanaokimbia mateso kutafuta hifadhi inazidi kutiliwa shaka, kuwekewa vikwazo au kunyimwa.

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha miaka 75 tangu kupitishwa kwa mkataba huo, Guterres amesema migogoro inaongezeka, mateso yanaendelea na idadi kubwa zaidi ya watu inalazimika kukimbia makazi yao.

“Mkataba wa Wakimbizi si masalia ya enzi nyingine. Ungali unahitajika leo kama ulivyohitajika wakati ulipopitishwa,” amesema Katibu Mkuu wa UN.

Mkataba huo ulipitishwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wakati mataifa yalipoahidi kuwa mtu anayekimbia mateso hatarudishwa mahali ambako maisha au uhuru wake unaweza kuwa hatarini kwa sababu ya rangi, dini, utaifa, uanachama wa kundi fulani la kijamii au maoni ya kisiasa.

Kwa mujibu wa Guterres, ahadi hiyo ilipopatiwa nguvu ya kisheria kupitia Mkataba wa mwaka 1951, iliokoa mamilioni ya maisha na kuwa moja ya vielelezo vya wazi zaidi vya ubinadamu wa pamoja.

Amesisitiza kwa kusema: “mkataba huo si kikwazo cha kukwepwa, bali ni msingi unaopaswa kulindwa kwa kuhakikisha watu wanapata ulinzi, taratibu za hifadhi zinaendeshwa kwa haki na utu, na kanuni ya kutomrudisha mtu mahali ambako anaweza kukabiliwa na mateso inaheshimiwa bila ubaguzi.”

Guterres amezitaka nchi kukataa sera zinazohamishia mataifa mengine wajibu wa kuwalinda wakimbizi, kuwaadhibu watu kwa sababu ya kutafuta usalama au kuweka masharti ya ulinzi kwa kuzingatia utaifa, dini, kabila au njia waliyotumia kuwasili.

Amesisitizia pia umuhimu wa ushirikiano wa kweli wa kimataifa na kugawana wajibu, ikiwemo kuzisaidia nchi na jamii zinazohifadhi idadi kubwa zaidi ya wakimbizi, ambazo nyingi zina rasilimali chache.

“Mkataba wa Wakimbizi ulizaliwa kutokana na kushindwa kwa ubinadamu kuwalinda watu wakati walipohitaji msaada zaidi. Tunapoadhimisha miaka 75, hatupaswi kuhatarisha kurudia kushindwa huko,” amesisitiza Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa…/