Dec 08, 2023 07:27 UTC
  • Kushadidi siasa za serikali ya Uingereza dhidi ya wahajiri

Kuongezeka maombi ya kutafuta hifadhi katika nchi za Ulaya, kumezifanya nchi hizo ziweka sheria kali za kupokea wahamiaji na wanaotafuta hifadhi, suala ambalo limezidisha mashinikizo dhidi yao.

Kuhusiana na jambo hilo, James Cleverly, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza amefanya safari nchini Rwanda ili kutia saini mkataba mpya kuhusiana na kuhamishiwa wakimbizi nchini humo. Mpango wa kuhamishiwa wakimbizi nchini Rwanda ni moja ya misingi mikuu ya mkakati wa serikali ya kihafidhina ya Rishi Sonak, Waziri Mkuu wa Uingereza, wa kukabiliana na wahamiaji haramu na kupunguza idadi ya wakimbizi wanaopitia Kanali ya La Manche kuingia Uingereza.

Suala la kuwahamishia wakimbizi wa Uingereza nchini Rwanda limekuwa likizungumziwa kwa miezi kadhaa na makubaliano yametiwa saini na serikali za nchi hizo ili kuwezesha wahamiaji na wanaotafuta hifadhi nchini Uingereza wahamishwe moja kwa moja hadi Rwanda. Uamuzi wa Waingereza kupeleka wanaoomba hifadhi katika nchi ya tatu umekuwa na utata mkubwa. Wengi wanaichukulia Rwanda kuwa nchi isiyo salama na wanasema kupelekwa Afrika Mashariki wakimbizi ambao wengi wao wanatoka katika familia zenye kipato cha chini kunahatarisha maisha na afya zao. Wengi pia wanaamini kuwa uamuzi huo utaigharimu sana Uingereza kwa sababu wakimbizi wengi watapaswa kusafirishwa kwa ndege hadi Afrika Mashariki.

Kufuatia malalamiko mengo yaliyotolewa katika uwanja huo, safari ya kwanza ya ndege ya wakimbizi wa Uingereza waliokuwa wamelazimishwa kuhamia Rwanda ilisimamishwa Juni 14 kwa amri ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu. Hata hivyo, serikali ya Uingereza bado inatilia mkazo juu mpango huo na safari ya hivi sasa ya Cleverly inasisitiza udharura wa kutekelezwa mpango huo. Mapatano ya sasa kati ya nchi mbili yanailazimisha Rwanda kutowafukuza wakimbizi wanaotumwa nchini humo na Uingereza.

Jitihada za Uingereza za kuwahamishia wakimbizi Rwanda

Mpango wa Uingereza wa kuwahamishia nchini Rwanda wakimbizi ulitangazwa kwa mara ya kwanza na Boris Johnson, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, mpango ambao umekosolewa vikali na vyama na mashirika ya haki za binadamu baada ya kutekelezwa na serikali ya Sunak. Wakosoaji wa mpango huo, ikiwa ni pamoja na vyama vya upinzani na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, wanaamini kwamba mpango huo hauna maana na unakwenda kinyume na maadili.

Lakini serikali ya Sunak inatilia mkazo sana kutekelezwa kwake ikidai kuwa ni njia ya kudhibiti wanaotafuta hifadhi na wahamiaji haramu nchini Uingereza. Robert Jenrick, Naibu Katibu wa Masuala ya Uhamiaji katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza, hivi karibuni alisema katika muktadha huo: 'Kuondoka katika Umoja wa Ulaya kulitupa fursa ya kutojihusisha na mikataba inayohusiana na sheria za uhamiaji.'  Suela Braverman, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza aliyeuzuliwa, pia alisema kuwa ndoto yake ni kuona picha ya ndege ya kwanza inayochukua wahamiaji kutoka Uingereza kuwapeleka Rwanda; ndoto ambayo sasa inatimia taratibu kufuatia ziara ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza nchini Rwanda.

Mbali na Uingereza, wahamiaji na wanaotafuta hifadhi katika nchi nyingine za Ulaya pia wako chini ya mashinikizo makubwa kama hayo. Italia ni miongozi mwa nchi ambazo zimeweka sheria ngumu za  kuwapokea wanaoomba hifadhi na hata kukubali raia wa kigeni walioingia kihalali nchini humo.

Wahajiri wanaohatarisha maisha yao kwa ajili ya kufika Ulaya

Kulingana na sheria ya serikali ya Italia inayotarajiwa kupasishwa na baraza la mawaziri la nchi hiyo,  wageni wanaoishi kihalali nchini Italia wanaweza kufukuzwa ikiwa serikali itawaona kuwa tishio kwa amani na usalama  wa taifa hilo. Sheria hiyo inaonyesha nia ya serikali ya Italia ya kupunguza idadi ya wahamiaji wanaofika katika pwani ya nchi hiyo. Nchini Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya, sheria kali dhidi ya wahamiaji na wanaotafuta hifadhi zimeongezeka. Pamoja na hayo lakini mamia ya raia wa Asia Magharibi na Afrika bado wanafanya juhudi kubwa za kufika katika mipaka ya Ulaya.

Tags