Mgogoro wa kisiasa Tunisia wazidi kutokota, Rais awatimua maafisa wengine wa serikali
(last modified Thu, 29 Jul 2021 11:05:12 GMT )
Jul 29, 2021 11:05 UTC
  • Mgogoro wa kisiasa Tunisia wazidi kutokota, Rais awatimua maafisa wengine wa serikali

Tunisia imeendelea kutumbukia zaidi katika mgogoro mkubwa wa kisiasa baada ya Rais Kais Saied kuwafukuza kazi maafisa zaidi, siku chache tu baada ya kumtimua waziri mkuu, kusimamisha shughuli za Bunge na kuchukua madaraka yote ya kiutawala.

Baada ya kusimamisha Bunge na kumtimua Waziri Mkuu Hichem Mechichi Jumapili iliyopita, na vilevile kuwafukuza mawaziri wa ulinzi na sheria siku moja baadaye, Saied ameamuru kufutwa kazi maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa serikali ya Tunis.

Rais huyo wa Tunisia mwenye umri wa miaka 63, mhadhiri wa zamani wa sheria na mwanagenzi wa kisiasa ambaye alishinda kwa kishindo uchaguzi wa urais wa 2019, ametoa amri ya kufukuzwa orodha ndefu ya maafisa wakuu wa serikali, pamoja na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Jeshi.

Jana Jumatano pia alimtimua Mkurugenzi Mtendaji wa runinga ya taifa ya al Wataniya.

Vilevile ameondoa kinga ya wabunge na kuchukua mamlaka ya kimahakama. Aidha ameamuru kufanyika uchunguzi dhidi ya vyama vitatu vya kisiasa kwa tuhuma za kupokea fedha kutoka nje ya nchi kabla ya uchaguzi wa 2019.

Maamuzi hayo ya Rais Kais Saied wa Tunisia yamepingwa vikali na vyama vya upinzani na wanaharakati wa masuala ya siasa. 

Kais Saied

Chama cha Ennahdha, ambacho kilikuwa kikundi kikubwa zaidi katika serikali ya mseto ya Tunis, kimeyata maamuzi hayo kuwa ni "unyakuzi wa madaraka"

Ali al-Aridh, Naibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Ennahdha ametangaza kuwa, maamuzi yaliyotangazwa na Rais Kais Saied ni mapinduzi dhidi ya asasi za serikali, katiba na mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo. 

Weledi wa mambo wanasema kuwa, hatua hiyo inaweza kuitumbukiza Tunisia katika mgogoro mkubwa kabisa wa kisiasa ambao haujawahi kushuhudiwa tangu alipoondolewa madarakani kwa vuguvugu la wananchi Zeinul Abidin bin Ali mwaka 2011.

Tags