Jeshi la Somalia laua zaidi ya magaidi 37 wa al-Shabaab
Kikosi maalum cha Danab cha Jeshi la Somalia kimewaua zaidi ya wanamgambo 37 wa kundi la al-Shabaab katika kijiji cha Maqooqaha, kilichoko magharibi mwa Buulo Xaaji katika eneo la Lower Jubba, kusini mwa nchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Ulinzi, operesheni hiyo ilifanyika Jumamosi na ilikuwa imepangwa kwa umakini mkubwa, ikilenga makamanda wa juu wa al-Shabaab.
Wizara ilisema kuwa jeshi, na hasa vikosi maalum vya Danab, vitaendelea na kampeni pana ya kulitokomeza kundi la al-Shabaab, ikiwa ni ushahidi wa dhahiri wa “ahadi isiyoyumba” ya majeshi ya Somalia katika kulinda taifa, raia na kuleta uthabiti wa kudumu.
“Mapambano dhidi ya al-Shabaab yataendelea kwa nguvu katika kila upande,” imesisitiza Wizara ya Ulinzi.
Kwa zaidi ya miaka 16, Somalia imekuwa ikikumbwa na ukosefu wa usalama, huku makundi ya kigaidi kama al-Shabaab na ISIS (Daesh) yakihatarisha maisha ya raia, maafisa wa serikali na wanajeshi.
Al-Shabaab, kundi lenye uhusiano na al-Qaeda, limekuwa likiendesha uasi dhidi ya serikali, likitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya viongozi wa serikali, maeneo ya kijeshi, na miundombinu ya umma.