Marekani yaiuzia Israel silaha zaidi kuendeleza mauaji ya kimbari Gaza
Serikali ya Marekani imeidhinisha mauzo ya silaha yenye thamani ya dola milioni 510 kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, ikiwa ni muendelezo wa uungwaji mkono wa kijeshi wa Washington wakati mauaji ya kimbari yanayoendeshwa na Israel dhidi ya watu wa Gaza yanaingia mwezi wa 21.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa uhamisho huo wa silaha unalenga “kuiwezesha Israel kuendeleza na kudumisha uwezo imara wa kijeshi,” ikidai kuwa ni “muhimu kwa maslahi ya usalama wa taifa wa Marekani.”
Mkataba huo wa silaha uliidhinishwa kupitia mpango wa Uuzaji wa Zana za Kijeshi kwa Nchi za Kigeni na kutangazwa rasmi kwa Bunge la Marekani siku ya Jumatatu.
Serikali ya Marekani imedai kuwa mauzo haya "hayatabadilisha usawa wa kijeshi wa msingi katika eneo la Mashariki ya Kati."
Mnamo Februari, wizara hiyo ilitangaza kuidhinisha mauzo ya silaha zaidi ya dola bilioni 7.4 kwa Israel, ambayo tayari imetumia silaha hizo hatari kutoka Marekani katika vita vyake vya maangamizi na mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza.
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel, alimsifu Rais Trump wa Marekani mapema mwaka huu kwa kusema: “Donald Trump ni rafiki mkubwa zaidi ambaye Israel imewahi kuwa naye katika Ikulu ya Marekani. Ameonyesha hilo kwa kututumia silaha zote zilizokuwa zimekwama.”
Tangu Oktoba 7, 2023, wakati utawala wa Kizayuni ulipoanzisha kampeni yake ya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza, takriban Wapalestina 56,674 wameuawa na 134,105 kujeruhiwa, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza. Makadirio mengine yanataja idadi hiyo kuwa ni zaidi ya Wapalestina 100,000 waliouawa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Licha ya ukosoaji mkubwa wa kimataifa kuhusu uhalifu wa Israel dhidi ya binadamu huko Gaza, Marekani inaendelea kuipatia silaha na msaada wa kijeshi, ikipuuza maonyo kuwa uungwaji mkono huo unaifanya kuwa mshirika katika vita hivyo vya maangamizi na uharibifu.