Serikali ya Tanzania yakanusha madai ya kupanga kumpa sumu Tundu Lissu
Serikali ya Tanzania imekanusha vikali tuhuma zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kudai kuwa zinaihusisha yenyewe na kiongozi wa upinzani, Tundu Antipas Lissu, katika mpango wa kumuwekea sumu mshtakiwa huyo.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa Julai 3, 2025, na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Serikali imetoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa hizo, ikisisitiza kuwa "hazina ukweli wowote."
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amefafanua kuwa Tundu Antipas Lissu, ambaye anatajwa na wanaharakati hao nje ya nchi na pia katika taarifa ya chama chake cha siasa, anakabiliwa na mashtaka Mahakamani. Mbali na mashataka ya uchochezi, Lissu anakabiliwa na shitaka la uhaini, ambalo halina dhamana na kama akikutwa na hatia adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.
Taarifa ya Msigwa inasema kuwa, Lissu anashikiliwa gerezani mpaka hapo shauri lake litakapohitimishwa Mahakamani. Serikali imesisitiza kuwa "haijawahi kuwa na mpango wa kumwekea sumu mtu yeyote aliyepo gerezani wala haina mpango wa kufanya hivyo kwa mtu yeyote."
Imetaja taarifa hizo kuwa "nia ovu ya kuchafua sifa na heshima kubwa ya Tanzania" na kwamba mamlaka zimeanza kuchukua hatua kali dhidi ya waliohusika na kuchapisha na kusambaza "uongo huo."
Tundu Lissu ambaye ni Mwenyekiti Taifa wa Chama Kikuu cha uopinzani nchini Tanzania cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA alipandishwa kizimbani hivi karibuni kwa tuhuma za uhaini; shitaka ambalo hukumu yake ni kifo, kwa matamshi yake aliyoyatoa ambayo waendesha mashtaka walisema alitoa wito kwa umma kuanzisha uasi na kuvuruga uchaguzi ujao.