Waasi wa M23: Tuko tayari kushiriki mazungumzo ya amani ya Doha
(last modified Fri, 04 Jul 2025 07:12:37 GMT )
Jul 04, 2025 07:12 UTC
  • Waasi wa M23: Tuko tayari kushiriki mazungumzo ya amani ya Doha

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na waasi wa M23 wamesema kwamba watatuma wajumbe nchini Qatar kwa mazungumzo ya amani, huku Washington ikishinikiza kukomeshwa kwa mapigano ambayo yanaweza kusaidia kufungua mabilioni ya uwekezaji katika madini.

M23 inashikilia eneo kubwa zaidi kuliko hapo awali mashariki mwa Congo baada ya kufanya harakati za mapema mwaka huu.

Mapigano hayo, ambayo ni machafuko ya hivi punde katika mzozo wenye chimbuko la mauaji ya halaiki ya Rwanda miongo mitatu iliyopita, yamewaua maelfu ya watu na kuwafanya mamia kwa maelfu kuyahama makazi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Waziri wa Mambo ya nje wa DRC Therese Kayikwamba Wagner alisema: "Haya ni mazungumzo ambayo yalifanyika ndani ya mfumo wa mchakato wa Doha na ambayo lazima yaendelee ndani ya mfumo wa mchakato wa Doha. Hatutatoa maoni juu ya hilo.

Aliongeza kuwa: ‘’Tumeshughulikia michakato yote, iwe mchakato wa Luanda, mchakato wa Washington DC, au mchakato wa Doha, kwa taaluma sawa na heshima kwa mwezeshaji, kwa busara, hasa kuchangia mazingira yanayofaa kwa ajili ya majadiliano yenye kuzaa matunda. Tutadumisha msimamo huu. Mazungumzo haya yalifanyika Doha na yataendelea Doha.

Tangu mwanzoni mwa Januari 2025, waasi wa M23 wamechukua udhibiti wa maeneo kadhaa ya mashariki mwa Kongo, ikiwa ni pamoja na miji ya Goma na Bukavu, na wanaendelea kusonga mbele. Viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wainaishutumu Rwanda kwamba inawaunga mkono waasi hao, lakini serikali ya Rwanda inakanusha tuhuma hizo na kusema kwamba kundi hilo linafanya kazi chini ya himaya ya serikali ya Kinshasa.