Maandamano Uturuki ya kulaani katuni za kumvunjia heshima Mtume (SAW)
(last modified Thu, 03 Jul 2025 12:06:41 GMT )
Jul 03, 2025 12:06 UTC
  • Maandamano Uturuki ya kulaani katuni za kumvunjia heshima Mtume (SAW)

Mamlaka za Uturuki zimesema kuwa, zimeanzisha uchunguzi kuhusu kuchapishwa kwa katuni inayohusishwa na Mtume Muhammad (SAW) na jarida la Leman, na wamemkamata mchora katuni, mhariri mkuu wa jarida hilo, na mkuu wa taasisi hiyo.

Watu waliokamatwa wameshtakiwa kwa "kutusi maadili ya kidini hadharani."

Gazeti hilo lilikanusha vikali madai hayo katika taarifa yake. "Picha hiyo haimuashirii Mtume wa Uislamu," ilisema taarifa ya jarida hilo.

Kufuatia msukosuko kwenye mitandao ya kijamii kuhusu katuni hiyo, video zilitolewa zikionyesha umati mkubwa wa watu uliokusanyika mbele ya jengo la jarida hilo, wakiimba "Idumu Sharia," wakiomba, na kuimba takbira.

Polisi waliwazuia waandamanaji waliokuwa wakijaribu kuingia katika jengo la gazeti hilo.

Waandamanaji hao waliokuwa na hasira walipaza sauti kulaani hatua ya jarida hilo ya kumvunjia heshima Mtume (SAW) na kutoa mwito wa wahusika kuchukuliwa hatua.

Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Istanbul ilisema kwamba amri imetolewa kukusanya toleo la hivi punde la jarida la vichekesho la Leman na mchakato wa kuzuia akaunti za mitandao ya kijamii za jarida hilo pia umeanza.

Katika toleo lililochapishwa Juni 26 mwaka huuu, wahusika wawili wanaoitwa Muhammad na Moses wanasalimiana wanapoingia katika jiji lililoshambuliwa kwa mabomu.

Waziri wa Sheria wa Uturuki alitangaza kuwa uchunguzi wa mahakama umeanzishwa dhidi ya jarida hilo chini ya Kifungu cha 216 cha Kanuni ya Adhabu ya Uturuki.