WHO: Mfumo wa afya Gaza unakabiliwa na hatari ya kusimama kikamilifu
(last modified Thu, 03 Jul 2025 12:04:45 GMT )
Jul 03, 2025 12:04 UTC
  • WHO: Mfumo wa afya Gaza unakabiliwa na hatari ya kusimama kikamilifu

Shirika la Afya Duniani  (WHO) limeonya kuwa, mfumo wa afya katika Ukanda wa Gaza unakabiliwa na hatari ya kusimama kikamilifu kutokana na uhaba wa nishati, kwani hakuna shehena ya mafuta iliyoingiakatika ukanda huo kwa zaidi ya siku miezi mitatu sasa.

Shirika  hilo lilithibitisha katika chapisho lake kwenye mtanmdao wa kijamii wa "X" kwamba, uhaba huu umesababisha kupooza na kusimama kwa shughuli za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na huduma za afya na hivyo kusukuma hospitali kwenye ukingo wa kusambaratika.

Kwa kuzingatia mashambulizi ya mabomu yanayoendelea na kuongezeka kwa idadi ya waliojeruhiwa, hospitali zinatatizika kutoa huduma za kimsingi za kuokoa maisha ya wagonjwa na majeruhi.

Shirika hilo limedokeza kuwa, akiba ya mafuta iliyopo inatosha kuhudumia kwa kiwango fulani hospitali 17 kwa muda mfupi tu, huku kiasi kinachopatikana kutoka katikka hifadhi ya mafuta ya Umoja wa Mataifa kiko katika eneo ambalo ni vigumu kufikiwa.

Mkurugenzi wa hospitali ya Al-Shifa huko Gaza, Muhammad Abu Salmiya, ameonya kuwa, sekta ya afya inapitia nyakati ngumu, na hospitali zinaweza kugeuka kuwa makaburi badala ya mahali pa kuokoa wagonjwa kutokana na ukosefu wa mafuta yanayohitajika kuendesha jenereta za umeme.

Wizara ya Afya huko Gaza pia imeonya mara kadhaa juu ya kukatizwa kwa huduma zake muhimu kutokana na kufungwa kwa vivuko na kuzuiwa kuingia kwa misaada katika eneo hilo.

Shirika hilo limetoa wito wa kuingizwa mara moja kwa mafuta katika Ukanda wa Gaza ili kuepusha janga la kiafya, likionya kuwa kuendelea kwa hali ya sasa kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa maisha ya wagonjwa na majeruhi.