Kwa nini shambulio la Israel na Marekani dhidi ya Iran limetoa pigo kubwa kwa NPT?
(last modified Thu, 03 Jul 2025 07:26:25 GMT )
Jul 03, 2025 07:26 UTC
  • Kwa nini shambulio la Israel na Marekani dhidi ya Iran limetoa pigo kubwa kwa NPT?

Tovuti ya Kiingereza ya Al Jazeera imezungumzia matokeo ya hujuma za karibuni za Marekani na Wazayuni katika ardhi ya Iran na vituo vyake vya nyuklia, na kuandika kwamba vita vya siku 12 havijafanikiwa chochote isipokuwa kuharibu uaminifu wa kiwango fulani uliokuwepo kuhusiana na Mkataba wa Kuzuia Usambazaji wa Nyuklia (NPT).

Natija ambayo sasa nchi nyingi zimeifikia kutokana na vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel pamoja na Marekani ni kwamba, kuwa mwanachama wa NPT sio hakikisho tena la kudhaminiwa usalama wa nyuklia.

Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza ushindi wa haraka baada ya kulipua vituo vya nyuklia vya Iran, huku utawala wake ukidai kuwa "dunia sasa ni mahala salama zaidi baada ya shambulio hilo kuharibu uwezo wa Iran wa eti kutengeneza silaha za nyuklia." Ingawa kiwango cha uharibifu wa mpango wa nyuklia wa Iran bado hakijajulikana, lakini mfumo uliokuwa ukidhibiti usambazaji wa silaha za nyuklia na ambao umekuwa ukisimamia na kuweka wazi shughuli za mpango huo kwa miaka mingi sasa umesambaratika.

Al Jazeera ya Kiingereza imesisitiza kwamba hatua hii ya kijeshi yenye mtazamo finyu, badala ya kudhibiti kuenea kwa silaha za nyuklia, inaweza kuongeza tishio la nyuklia ambalo lilikusudiwa kudhibitiwa na mfumo huo, na hivyo kuhatarisha usalama wa sio tu Asia Magharibi, bali ulimwengu mzimai. Kwa hakika, kwa kulipua vituo vinavyosimamiwa na IAEA, Marekani imeyathibitishia mataifa yasiyo na silaha za nyuklia kwamba ushirikiano na chombo hicho cha usimamizi cha Umoja wa Mataifa hahuyadhaminii usalama wowote. Hii ni katika hali ambayo mpango mzima wa nyuklia wa Iran umekuwa ukifuatiliwa na kusimamiwa kwa karibu na kwa miongo kadhaa na wakala wa IAEA.

Hatua ya Marekani na Israel ya kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran, katika hali ambayo Iran bado ni mwanachama hai wa NPT, imepelekea bunge la Iran kupitisha sheria ya kusimamisha kwa muda ushirikiano wowote na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.

Mkataba wa NPT

Donald Trump, Rais mtatanishi wa Marekani ambaye aliihudumia pakubwa Israel katika muhula wake wa kwanza, amekuwa akiunga mkono sera na vitendo vya uadui vya utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Iran tangu mwanzoni mwa uongozi wake Januari mwaka huu, ambapo sio tu inatekeleza kampeni ya mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran, bali pia amekuwa akifanya mazungumzo ya kidhahiri tu na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia na wakati huo huo kuidhinisha mashambulio ya kijeshi yafanyike dhidi yake. Kuhusiana na hilo, alirudia matakwa yake ya awali kwa kumtumia barua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambayo hatimaye ilipelekea kufanyika duru tano za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, yakipatanishwa na Oman.

Wakati duru ya sita ya mazungumzo hayo ilipangwa kufanyika tarehe 15 Juni, utawala wa Kizayuni kwa mipango na ushirikiano wa Marekani, ulifanya mashambulizi ya anga dhidi ya shabaha mbalimbali nchini Iran asubuhi ya Ijumaa, Juni 13. Katika mashambulizi hayo haramu ambayo yalikiuka wazi Hati ya Umoja wa Mataifa, maeneo ya kijeshi, vituo vya nyuklia na makazi ya Iran yalilengwa, na kupelekea kuuawa shahidi makamanda wa ngazi za juu wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, wanajeshi na wasio wanajeshi. Kisha, asubuhi ya Jumapili, Juni 22, Marekani ilishambulia maeneo ya urutubishaji urani ya Natanz na Fordow na kituo cha nyuklia cha Isfahan. Awali, vituo hivi, pamoja na kituo cha maji mazito na kinu cha nyuklia kinachoendelea kujengwa huko Khandab Arak, vilikuwa tayari vimelengwa katika mashambulio ya anga ya Israel.

Jambo la kuzingatiwa ni kwamba, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel, katika taarifa yake baada ya mashambulizi ya utawala huo dhidi ya Iran, alidai kwa jazba kwamba operesheni ya utawala huo ililenga kuharibu miundombinu ya nyuklia na makombora ya Iran. Hii ni pamoja na ukweli kwamba kwa mujibu wa sheria za kimataifa ni marufuku kushambulia na kuharibu vituo vya nyuklia, ambapo hata katika vita na migogoro ya baada ya Vita vya Pili vya Dunia, isipokuwa wakati wa vita vya Ukraine na katika hali nadra sana, hakuna upande wowote katika migogoro hiyo uliojaribu kushambulia miundombinu ya nyuklia.

Israel imeshambulia vituo vya nyuklia vya Iran kwa kisingizio kuwa inajaribu kuunda silaha za nyuklia, ingawa yenyewe ina rundiko kubwa la silaha za nyuklia. Utawala wa Kizayuni unaripotiwa kuwa na vichwa 75 hadi 200 vya nyuklia lakini pamoja na hayo hauruhusu ukaguzi wa kimataifa kufanyika katika vituo vyake vya nyuklia. Licha ya ukweli kwamba nchi za eneo mara zote zimetoa wito wa Mashariki ya Kati kutokuwa na silaha za nyuklia, lakini utawala huo umepuuza suala hilo na unaendelea kujirundukia silaha hizo hatari. Licha ya kuwa mwanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, lakini Israel imekataa kujiunga na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), wakati Iran ni mwanachama kamili wa mkataba huo tangu 1970.

Kituo cha Nyuklia cha Fordow

Kwa mukhtasari, ni kuwa mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran yameanzisha uzushi hatari; ikimaanisha kwamba ingawa Iran ilifungua vituo vyake vya nyuklia kwa wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na kubakia ndani ya mfumo wa mazungumzo, lakini imeshambuliwa kijeshi. Iwapo nchi nyingine zitafikia natija kuwa kuheshimu mkataba wa NPT na kuruhusu ukaguzi ufanyike kwenye vituo vyao vya nyuklia hakutazilinda dhidi ya mashambulizi na vitisho, basi njia pekee ya kujidhaminia usalama ni kubuni kizuizi cha nyuklia. Kwa mfano, Marekani iliacha kufikiria kushambulia vituo vya nyuklia vya Korea Kaskazini baada ya nchi hiyo kujipatia silaha za nyuklia.

Kwa hivyo, dhihirisho hili la ubabe na utumiaji mabavu la Marekani na Israel, katika kuvishambulia vituo vya nyuklia vya Iran, hata kama litarudisha nyuma kwa muda mpango wa nyuklia wa Iran, lakini sasa limehatarisha mkataba wa NPT na utulivu wa eneo. Ni wazi kuwa, mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo vya amani vya nyuklia vya Iran ni makosa makubwa ya kistratijia.