Iran yaghariki katika maomboleza ya Tasua ya Imam Hussein AS
Mamilioni ya Waislamu nchini Iran wamejiunga na wenzao duniani kote kuadhimisha Tasu'a, siku moja kabla ya maadhimisho ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW).
Wairani katika mji mkuu Tehran, majiji, miji na vijiji vyote nchini leo Jumamosi wamekusanyika misikitini katika na vituo vya kidini, huku baadhi wakiingia barabarani kuadhimisha marasimu hayo makubwa ya kumuomboleza Imam Hussein AS.
Waombolezaji katika kona zote za Iran wametangaza kwa sauti kubwa utiifu wao kwa wanamapambano wa Karbala, huku wakijibari na kujiweka mbali na maadui wa Uislamu na wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran sanjari na kutoa mkono wa pole kwa Waislamu kote duniani ambao hii leo wapo katika maombelezo ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS, imeitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kivitendo za kusimamisha jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Katika siku ya 9 ya mwezi Muharram, waombolezaji humkumbuka zaidi Abul Fadhl Abbas bin Ali, ndugu yake Imam Hussein AS ambaye ndiye aliyekuwa mbeba bendera na kamanda wa jeshi la mtukufu huyo katika mapambano ya siku ya Ashura.

Alionesha ushujaa wa hali ya juu katika mapambano ya Karbala na kuwakumbusha watu ushujaa usio na kifani wa baba yake, Ali bin Abi Twalib (AS). Abul Fadhl Abbas aliuawa shahidi tarehe kumi Muharram baada ya kukatwa mikono miwili na maadui wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad SAW ambao kinara wao alikuwa ni Yazid bin Muawiyah.
Idhaa ya Kiswahili, Radio Tehran inatoa salamu za rambirambi kwa Waislamu wote hususan Mashia na wapenda uhuru wengine duniani kwa mnasaba wa siku hii ya Tasu'a ya Imam Hussein (AS).