Rais wa Kenya aonya kuhusu njama ya kupindua serikali kupitia maandamano
Rais wa Kenya William Ruto siku ya Jumatano aliwashutumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kupanga njama ya kupindua serikali yake, akionya kuwa mashambulizi dhidi ya vituo vya polisi na maandamano yenye vurugu yatatafsiriwa kama vitendo vya kivita.
Akizungumza katika Kituo cha Polisi cha Kilimani jijini Nairobi, wakati wa ukaguzi wa mradi wa makazi kwa maafisa wa polisi, Ruto alisema:
“Nataka kuwaambia wale wanaodhani wanaweza kubadilisha serikali hii kwa kutumia vurugu na njia zisizo halali kabla ya 2027, wajaribu!.”
Amesema: “Hii ni nchi ya kidemokrasia, na Wakenya watachagua uongozi kupitia kura. Hatuwezi kuchagua viongozi kwa kutumia vurugu. Hilo halitatokea katika nchi hii.”
Kauli zake zinakuja huku maandamano dhidi ya serikali yakiongezeka kote Kenya katika wiki za hivi karibuni yakichochewa na wanasiasa wa upinzani wanatumia vibaya malalamiko ya wananchi kuhusu ukatili wa polisi na hali ngumu ya kiuchumi.
Katika siku za hivi karibuni, waandamanaji wameripotiwa kuvamia vituo vya polisi na kukabiliana na vikosi vya usalama, huku video zikisambaa mtandaoni zikionesha hali ya machafuko katika maeneo mbalimbali.
Ruto, akiwa na hasira dhahiri, aliwatuhumu baadhi ya waandamanaji kuwa wanafadhiliwa na wapinzani wa kisiasa, na akaapa kuchukua hatua kali.
Aliweka wazi kuwa shambulizi lolote dhidi ya kituo cha polisi litachukuliwa kama jaribio la uasi.
Amesema: “Mtu yeyote anayeshambulia kituo cha polisi nchini Kenya… hiyo ni tangazo la vita. Hali hiyo haitavumiliwa. Imetosha sasa. Nitawalinda wananchi na mali yao.”
Rais Ruto amongeza kuwa: “Nitatumia kila mbinu inayopatikana ili kudumisha utulivu wa nchi na kulinda serikali dhidi ya njama haramu zinazolenga kuvuruga demokrasia.”
Onyo hili linajiri siku chache baada ya maandamano ya kumbukumbu ya Saba Saba, ambapo watu 31 waliripotiwa kuuawa kwa mikono ya polisi, na zaidi ya 500 kukamatwa.