Hunter Biden: Netanyahu anataka kuchochea vita ili kuhepa kuswekwa jela
Hunter Biden mwana wa kiume wa Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden amemkosoa vikali Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni.
Hunter Biden amemfananisha Netanyahu na mnyama mkubwa ambaye anakabiliwa na upungufu wa uungaji mkono wa ndani; kwa msingi huo anafanya kila awezalo kushadidisha vita ili kuhepa kuhukumiwa na kufungwa jela.
Duru za habari za Israel zimeandika: "Hunter Biden, mtoto wa Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden, amelaani mauaji ya kimbari ya raia wa Palestina katika mahojiano yake na waandishi wa habari, na kuwataka wananchi wa Marekani wanaopinga jinai za utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza kuungana kote nchini kupinga kushiriki Marekani katika jinai za utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Hunter ameashiria kupungua sana uungaji mkono wa wakazi wa Israel kwa Waziri Mkuu huyo wa utawala wa kizayuni na kusema: Netanyahu analielekeza eneo la Mashariki ya Kati katika vita vingine badala ya kujinusuru. Hii ni kwa sababu ni asilimia 22 tu ya wakazi wa utawala wa Kizayuni ndio wanaomuunga mkono Waziri Mkuu huyo wa Israel.
Mtoto wa Joe Biden amesisitiza pia kuwa Netanyahu katika kipindi cha miaka 22 iliyopita alidai mara kadhaa kwamba Iran inakaribia kumiliki silaha za nyuklia hata hivyo amekuwa akikosea kila wakati, na amekuwa akitoa madai haya ili adumu katika medani ya siasa.