UNHCR yaonya juu ya ukandamizaji wa haki za wakimbizi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i140266-unhcr_yaonya_juu_ya_ukandamizaji_wa_haki_za_wakimbizi
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema haki za waomba hifadhi ulimwenguni zinakabiliwa na shinikizo kubwa la kisiasa. Hayo yameelezwa wakati shirika hilo likiadhimisha miaka 75 ya kupitishwa kwa Mkataba wa Wakimbiuzi.
(last modified 2026-07-30T04:11:28+00:00 )
Jul 30, 2026 04:04 UTC
  • UNHCR yaonya juu ya ukandamizaji wa haki za wakimbizi

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema haki za waomba hifadhi ulimwenguni zinakabiliwa na shinikizo kubwa la kisiasa. Hayo yameelezwa wakati shirika hilo likiadhimisha miaka 75 ya kupitishwa kwa Mkataba wa Wakimbiuzi.

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi ambako mkataba huo ulisainiwa Julai 28, 1951, kamishna wa UNHCR Barham Salih ametoa wito kwa ulimwengu kuacha kuzingatia tu ongezeko la wakimbizi na badala yake kutafutwe suluhisho la kudumu la tatizo hilo.

Kamishna Mkuu wa UNHCR amesema "Wakimbizi hawapaswi kutambulishwa kwa mazingira yaliyowalazimisha kukimbia makazi yao, bali kwa kile wanachoweza kuwa endapo watapewa fursa ya kujenga upya maisha yao. Na kuna ukweli mwingine ambao mara nyingi tunausahau: Wakimbizi wengi wanataka kurudi nyumbani kwao na hawataki kubaki wakimbizi milele."

Kabla ya hapo na kwa mnasaba wa maadhimisho hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alitoa wito kwa nchi zote wanachama kuhuisha dhamira yao ya kutekeleza Mkataba wa Wakimbizi wa mwaka 1951, akisema haki ya watu wanaokimbia mateso kutafuta hifadhi inazidi kutiliwa shaka, kuwekewa vikwazo au kunyimwa.

Kwa mujibu wa UNHCR, karibu watu milioni 117.8 kote ulimwenguni walilazimika kuyakimbia makazi yao hadi mwishoni mwa mwaka 2025, idadi iliyoshuka kiasi ikilinganishwa na rekodi ya mwaka 2024 ya watu milioni 123.2.

Hadi sasa Syria ndio taifa lenye wakimbizi wengi duniani ambao raia wake milioni 6 wamelazimika kuyakimbia makazi yao. Ukraine na Afghanistan zinafuatia. Barani Afrika Sudan inaongozwa kwa kuwa na wakimbizi wengi.