Hizbullah: Rekodi ya serikali ya Marekani imejaa umwagaji damu na jinai
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140874-hizbullah_rekodi_ya_serikali_ya_marekani_imejaa_umwagaji_damu_na_jinai
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imelaani vikali vikwazo vipya vya Wizara ya Hazina ya Marekani dhidi ya harakati hiyo.
(last modified 2026-08-22T12:20:13+00:00 )
Aug 22, 2026 12:19 UTC
  • Hizbullah: Rekodi ya serikali ya Marekani imejaa umwagaji damu na jinai
    Hizbullah: Rekodi ya serikali ya Marekani imejaa umwagaji damu na jinai

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imelaani vikali vikwazo vipya vya Wizara ya Hazina ya Marekani dhidi ya harakati hiyo.

Taarifa ya harakati hiyo ya Muqawama imesisitiza kuwa, serikali ya Marekani kutokana na historia yake ya umwagaji damu na kutenda jinai haina sifa wala uhalali wa kuchukua hatua kama hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Quds (Qudsna), likinukuu Al Mayadeen, Harakati ya Muqawama ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imetoa taarifa kali kulaani hatua ya uhasama ya Wizara ya Hazina ya Marekani ya kuiwekea harakati hiyo vikwazo vipya. Hizbullah imesema katika taarifa yake hiyo kwamba:

Madai ya serikali ya Marekani kwamba Hizbullah iko chini ya udhibiti wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ni kisingizio cha kuirejesha Hizbullah kwenye orodha ya vikwazo. Hatua hii ni sehemu ya mfululizo wa sera za serikali za Marekani zinazolenga kuishambulia, kuizingira na kuiwekea shinikizo Muqawama, mazingira yake ya kijamii na waungaji mkono wake.

Hizbullah imeongeza kuwa, vikwazo hivyo vipya vya Marekani vimewekwa kwa lengo la kulinda usalama wa adui, kuimarisha uvamizi kusini mwa Lebanon na kuweka mazingira ya kutekelezwa miradi yake ya upanuzi.

Taarifa hiyo imesema hatua hiyo inathibitisha kwamba, serikali ya Marekani, ambayo imezoea kutumia vikwazo ili kulazimisha utawala wake, bado inaichukulia Lebanon kwa mtazamo wa ulezi na uangalizi wa kigeni.

Hizbullah imesema pia kuwa, serikali ya Marekani inajaribu kuwazingira wananchi wa Lebanon, kuinyima Lebanon vyanzo vyake vya nguvu na kuchochea machafuko ya ndani nchini humo.