Rais Samia azindua mradi mkubwa utakaochangia nusu ya umeme unaozalishwa Tanzania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezindua Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere, hatua inayofungua rasmi kuanza kwa kazi ya mojawapo ya miradi mikubwa zaidi ya miundombinu nchini humo na mradi mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme unaofadhiliwa na serikali.
Akihutubia hafla ya uzinduzi huo uliofanyika leo, Rais Samia ametoa shukrani kwa serikali ya Misri iliyoshirikiana kwa karibu na Tanzania katika mradi huo akisema, hatua hiyo inaonyesha thamani ya ushirikiano barani Afrika kwa manufaa ya bara hilo.
"Hatua hii inaonyesha jinsi nchi zetu za Afrika, kwa kuungana na kushirikiana, zinavyoweza kufikia mambo makubwa kwa ajili ya ustawi wa watu wetu na bara zima," ameeleza Rais wa Tanzania.
Mradi huo, uliopo katika Mto Rufiji mkoani Pwani, una uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 na umeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Tanzania wa kuzalisha umeme.
Serikali inasema kituo hicho pekee kinachangia takriban asilimia 44.9 ya umeme wote unaozalishwa na kitaingiza umeme katika gridi ya taifa.
Mradi huo uligharimu takriban shilingi trilioni 7.452 za Tanzania, ikiwa ni sawa na karibu dola bilioni 3.35, na ulifadhiliwa na serikali ya Tanzania. Ujenzi ulianza mwezi Juni 2019 na kukamilika mwezi Machi 2025.
Rais Samia amesema, imani kwa serikali na azma ya Watanzania vimesaidia kufanikisha mradi huo.
"Tunapofanya maamuzi yenye manufaa kwa taifa, hatupaswi kukata tamaa eti kwa sababu njia ya utekelezaji imekuwa ngumu; badala yake, lazima tuwe na ujasiri na msimamo thabiti wa kusimamia maono na maamuzi yetu katika kufikia malengo tuliyojiwekea," amesisitiza kiongozi huyo.
Mbali na uzalishaji wa umeme, bwawa hilo, lenye uwezo wa kuhifadhi takriban mita za ujazo bilioni 33 za maji, linatarajiwa pia kusaidia kudhibiti mafuriko katika Mto Rufiji, pamoja na kusaidia shughuli za umwagiliaji, utalii na matumizi mengine ya kibinadamu.
Serikali imeelezea mradi huo kama hatua muhimu kuelekea kupata umeme wa uhakika kwa kaya na viwanda, huku ikijenga uwezo mkubwa zaidi wa kusaidia uwekezaji na ukuaji wa uchumi.
Mradi huo pia umehusishwa na malengo ya Tanzania ya kuimarisha biashara ya umeme katika kanda ya mashariki mwa Afrika kadiri uwezo wake wa uzalishaji unavyoongezeka…/