Ndejembi aapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
-
Deogratius Ndejembi aapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Deogratius Ndejembi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameapishwa kushika wadhifa huo mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
Ndejembi aliteuliwa katika nafasi hiyo baada ya mtangulizi wake, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, kujiuzulu nafasi hiyo tarehe 26 mwezi huu; hatua iliyofungua nafasi ya uteuzi wa Makamu mpya wa Rais.
Ndejembi ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, George Mcheche Masaju katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wa kitaifa; wakishuhudia hatua hiyo muhimu katika uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kuapishwa Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni hatua rasmi ya kuanza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa uzoefu wa Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi katika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini na katika sekta binafsi utamsadia kutekeleza majukumu ya dhima hiyo aliyopewa.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Makamu huyo wa Rais; Rais Samia amesema cheo alichopewa Ndejembi ni dhamana, na amemtaka kukitumia kwa maslahi ya taifa na kumtanguliza mbele Mwenyezi Mungu.