Kwa nini Marekani ilisimamisha vita dhidi ya Iran baada ya wiki mbili?
Kufuatia wiki mbili za uhasama na baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuzungumzia uwezekano wa kupanua mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, mapigano kati ya pande hizi yalisimama ghafla.
Wiki iliyopita, Trump alikuwa ametishia kwamba Iran ingekabiliwa na mashambulizi makali na yasiyo na mfano wake. Ripoti za vyombo vya habari pia zilionyesha uwezekano wa mapigano kuongezeka na kuathiri miundombinu ya kiraia. Hata hivyo, Trump alilegeza msimamo wake wa vitisho, akidai kuwa alikusudia kutoa nafasi zaidi kwa diplomasia. Swali linalojitokeza sasa ni je, kwa nini Trump kwa mara nyingine tena ameachana na vitisho vyake na kusimamisha mwenendo wa mgogoro huu? Je, hatua hii inaashiria mwisho wa vita, au ni kusitisha mapigano kwa muda tu?
Sababu kuu lazima itafutwe katika hatua zinazochukuliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uwanja huo. Katika wiki mbili zilizopita, vikosi vya jeshi la Iran vimeonyesha mbinu tofauti za kivita, vikichukua hatua kwa weledi mkubwa zaidi kuliko ilivyokuwa wakati wa vita vya awali vya siku 12 na siku 40 mtawalia. Mashambulizi makali ya mfululizo yaliyofanywa na vikosi vya Iran dhidi ya kambi na maslahi ya Marekani katika eneo yaliiweka tena Tehran katika mkondo wa mashinikizo endelevu, hali inayokumbushia kipindi cha kilele cha mgogoro wa vita vya siku 40. Kufuatia ubadilishanaji wa mara kwa mara wa mashambulizi ya kijeshi kati ya Iran na Marekani, mwelekeo wa mgogoro huu umekuwa tena kwa maslahi ya Iran. Trump na utawala wa Marekani wamefikia uamuzi kuwa Iran haitasalimu amri katika vita vinavyoendelea bali itaendelea kufuatilia malengo yake kwa nguvu zaidi, na hali hii hatimaye haiendani na maslahi ya Marekani.
Sababu ya pili inahusu athari za vita kwenye soko la nishati. Kadiri mzozo ulivyoendelea na kushika kasi, soko la kimataifa la nishati liliathirika haraka. Bei ya mafuta, ambayo awali ilikuwa imeshuka kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano na kutiwa saini hati ya maelewano kati ya Iran na Marekani, jambo lililoupa ahueni uchumi wa Marekani, ilipanda tena haraka kuelekea kiwango cha dola 100 huku kukiwa na ongezeko la mashinikizo ya Iran kwa jeshi la Marekani. Kuendelea kwa hali hii kungeweza kusababisha madhara makubwa kwa uchumi wa Marekani na wa dunia kwa ujumla.
Sababu ya tatu ni kuingia Yemen katika mzozo huu. Kwa kuanzisha mashambulizi dhidi ya Saudi Arabia na kutishia kufunga Lango-Bahari la Bab-el-Mandab, Yemen ilileta mabadiliko mapya yaliyochangia pakubwa kupanda kwa bei ya mafuta duniani, hali ambayo ingeweza kuendelea kuathiri uchumi wa dunia. Kwa upande mwingine, Saudi Arabia haina nia ya kujiingiza katika vita hivi, na Trump anafahamu ukweli huu.
Sababu ya mwisho inahusu taathira za mafanikio ya Iran na kuathirika vibaya itibari ya Trump kuafutia kushindwa kwake katika makabiliano na Tehran. Nchini Marekani, jambo linaloweza kudhoofisha zaidi nafasi ya rais si Bunge, bali ni kuongezeka kwa idadi ya majeruhi na vifo vya wanajeshi, tatizo lililomkabili Lyndon B. Johnson wakati wa Vita vya Vietnam na Joe Biden katika vita vya Afghanistan. Kwa mtazamo huu, hali ya sasa katika eneo na kwenye Lango la Hormuz inaweza kumuweka Trump katika hali ngumu kama hiyo.
Kwa pamoja, mambo haya ndiyo yamepelekea kusitishwa kwa muda makali ya mapigano yaliyokuwa yakiendelea lakini hili halina maana ya kumalizika vita, kwa kutilia maanani tamaa, tabia mbaya na historia ya Marekani ya kukiuka ahadi zake na kutumia vibaya mazingira yanayojitokeza.