Shambulio la kombora la Yemen lailazimisha Israel ifunge anga yake
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kuwa, Israel imelazimika kufunga uwanja wa ndege wa Ben Gurion na anga yake katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kufuatia kuvurumishwa kwa kombora kutoka Yemen.
Kwa mujibu wa duru za kijeshi za Israel, kombora hilo lilirushwa kutoka Yemen kuelekea katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Kanali ya 12 ya Kizayuni imeripoti kuwa, anga ya Israel imefungwa kufuatia kuvurumishwa kwa kombora hilo la balestiki. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uwanja wa ndege wa Ben Gurion pia ulifungwa kutokana na shambulio hilo.
Vikosi vya ulinzi vya Yemen vimetangaza kuwa, vimetumia kombora la balestiki katika operesheni hiyo dhidi ya uwanja wa ndege wa Ben Gurion. Vimesema shambulio hilo la kombora "limefikia lengo lake kwa mafanikio" na kusababisha ving'ora vya tahadhari kuhinikiza katika miji na vitongoji katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na jina bandia la Israel.
Operesheni hiyo imewafanya mamilioni ya Wazayuni walazimike kukimbilia mafichoni na kwenye mahandaki, sanjari na kusimamisha safari zao za ndege kutokea uwanja wa ndege wa Ben Gurion.
Vikosi vya ulinzi vya Yemen vimeapa kustawisha nguvu na uwezo wake wa kijeshi na kushadidisha vita kwa ajili ya kuonyesha mshikamano na wananchi madhulumu wa Palestina. "Operesheni hizi zitaendelea hadi uvamizi dhidi ya Gaza utakapokoma na vizuizi kuondolewa”, imesisitiza taarifa ya vikosi hivyo.
Haya yanajiri siku chache baada ya Bandari ya Eilat ya utawala wa kizayuni wa Israel kutangaza kusitisha shughuli zake baada ya kushindwa kulipa madeni yake, kufuatia kushuka kwa mapato kulikosababishwa na mashambulizi ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen katika Bahari Nyekundu.