Kwa nini Marekani imejiondoa rasmi UNESCO?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128662-kwa_nini_marekani_imejiondoa_rasmi_unesco
Marekani ilitangaza Jumanne, Julai 22, kwamba imejiondoa rasmi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO.
(last modified 2025-07-23T08:58:11+00:00 )
Jul 23, 2025 08:58 UTC
  • Kwa nini Marekani imejiondoa rasmi UNESCO?

Marekani ilitangaza Jumanne, Julai 22, kwamba imejiondoa rasmi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO.

Nchi hiyo imetangaza kujiondoa katika shirika hilo ambalo huainisha na kutangaza maeneo ya urithi wa dunia, kwa madai kwamba linatekeleza siasa zilizo dhidi ya Israel na kuunga mkono "masuala yanayoibua migawanyiko."

Tammy Bruce, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ameituhumu UNESCO kwa kukuza "maswala ya kijamii na kitamaduni yenye migawanyiko" na kuzingatia sana maswala ya kiitikadi. Pia ameituhumu UNESCO kwa kuchukua msimamo dhidi ya Israel, hasa uamuzi wake wa kukubali Palestina kuwa mwanachama wa shirika hilo na kusema: "Uamuzi wa UNESCO wa kukubali "Nchi ya Palestina" kama mwanachama unaibua matatizo, unapingana na siasa za Marekani, na unaimarisha mazungumzo dhidi ya Israel ndani ya shirika hilo."

Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO ameelezea masikitiko yake juu ya uamuzi huo wa Marekani katika taarifa yake akisema: "Ninasikitika sana kuhusu uamuzi wa Donald Trump wa kuiondoa Marekani katika UNESCO, ambao utaanza kutekelezwa mwishoni mwa Desemba 2026. "Uamuzi huu unakinzana na kanuni za msingi za ushirikiano wa pande nyingi na unaweza kuathiri, kwanza kabisa, washirika wetu wengi nchini Marekani, jumuiya zinazofuatilia kusajili maeneo ya kiutamaduni katika orodha ya Urithi wa Dunia, Hadhi ya Miji yenye Ubunifu na Viti vya Vyuo Vikuu."

Katika upande wa pili utawala wa Kizayuni umekaribisha uamuzi huo na kuishukuru Washington kwa kile ulichokiita "uungaji mkono wa kimaadili na kiuongozi." Gideon Sa’ar, Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala huo, ameandika kwa hasira kubwa kwenye mtandao wa kijamii wa X kama ifuatavyo: "Hii ni hatua ya lazima iliyochukuliwa ili kuimarisha uadilifu na kutetea haki ya Israel ya kutendewa haki katika mfumo wa Umoja wa Mataifa, haki ambayo imekuwa ikikanyagwa mara kwa mara kutokana na ghiliba za kisiasa katika eneo hili."

Chuki ya Trump dhidi ya UNESCO

Hii si mara ya kwanzai kwa Marekani kujiondoa UNESCO. Rais Ronald Reagan aliiondoa Marekani kwenye shirika hilo katika miaka ya 1980, akilituhumu kuwa "la rushwa" na linalounga mkono Soviet, lakini ikajiunga tena na UNESCO chini ya Rais George W. Bush. Marekani na Israel zilisitisha ufadhili kwa UNESCO baada ya wanachama wa shirika hilo kupiga kura ya kuikubali Palestina kuwa mwanachama wake mwaka 2011. Utawala wa Trump uliamua mnamo Oktoba 2017 kujiondoa kabisa UNESCO, kuanzia Desemba 31, 2018, lakini Rais Joe Biden akarejesha tena uanachama wa Marekani katika shirika hilo mwezi Juni 2023. Hata hivyo, baada ya Trump kushinda tena uchaguzi mwaka 2024, ilitabiriwa kuwa Marekani ingejiondoa tena UNESCO wakati wa muhula wa pili wa Donald Trump.

Hatua hiyo ya utawala wa Trump, kwanza, inawiana na uungaji mkono wake mkubwa kwa utawala wa Kizayuni na mashinikizo dhidi ya UNESCO kwa upande mmoja, na pili, inaendana na mtazamo wake wa jumla wa kujiondoa katika mashirika na taasisi muhimu za kimataifa, pamoja na mikataba na makubaliano ya kimataifa ya pande kadhaa. Katika muhula wake wa kwanza madarakani, Trump aliiondoa Marekani katika taasisi na mikataba mingi ya kimataifa, kama vile Makubaliano ya Hali ya Hewa ya Paris, Mapatano ya Nyuklia ya JCPOA, Ushirikiano wa Trans-Pacific (TPP) na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, pamoja na mikataba ya kimataifa kama vile Mkataba wa Makombora ya Masafa ya Kati ya Nyuklia (INF) na Mkataba wa Anga Wazi.

Sababu ya Marekani kujiondoa UNESCO wakati wa muhula wa kwanza wa Trump ilikuwa ni kutokubaliana nchi hiyo na suala zima la Palestina. Ingawa Marekani ilisalia katika UNESCO kama nchi mwangalizi, haikulipa tena ada za uanachama wake katika shirika hilo wala kuruhusiwa kupiga kura ya kuchagua au kuchaguliwa katika Kamati ya Urithi wa Dunia.

Bila shaka, Marekani imekuwa na matatizo ya muda mrefu na UNESCO kutokana na siasa huru za shirika hilo, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono kwake haki za uanachama wa Palestina katika chombo hiki chenye mfungamano na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo Washington imetoa visingizio kadhaa vizivyo na msingi kuhusiana na suala hilo ikiwa ni pamoja na kwamba inataka mabadiliko ya kimsingi yafanyike katika Umoja wa Mataifa na taasisi zake tanzu mfano UNESCO pamoja na kuangaliwa upya bajeti ya shirika hilo la kimataifa na kushughulikia ongezeko la deni la wanachama wake. Lakini huu ni mwonekano wa nje tu wa suala hilo, ambapo ni wazi kuwa sababu hasa ya Marekani kujitoa katika UNESCO ni kutoridhishwa kwake na misimamo na hatua za shirika hilo za kuwaunga mkono Wapalestina, ikiwa ni pamoja na kukubaliwa uwanachama wa Palestina katika UNESCO, na pia kulaaniwa mara kwa mara kwa hatua za utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wa Wapalestina.