Kwa nini Grossi amekiri haki ya Iran ya kurutubisha urani?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136590-kwa_nini_grossi_amekiri_haki_ya_iran_ya_kurutubisha_urani
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amekiri kwamba, Iran kama nchi iliyotia saini Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), ina haki ya kurutubisha urani.
(last modified 2026-02-13T11:21:59+00:00 )
Feb 13, 2026 11:21 UTC
  • Kwa nini Grossi amekiri haki ya Iran ya kurutubisha urani?
    Kwa nini Grossi amekiri haki ya Iran ya kurutubisha urani?

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amekiri kwamba, Iran kama nchi iliyotia saini Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), ina haki ya kurutubisha urani.

Rafael Grossi amesema "makubaliano ya pande zote ndani ya mfumo wa (NPT) ni kwamba unaweza kufanya hivi, lakini unanipa ruhusa ili niweze kuchunguza kila gramu ya mwisho (ya urani) ambayo imefungwa na haijaelekezwa kwenye kitu kingine chochote."

Matamshi hayo ya Grossi ni muhimu kwa sababu mnamo Juni mwakla jana (2025), kwa kisingizio cha kutokubali ombi la Iran la kusimamisha kabisa mchakato wa urutubishaji urani wakati wa mazungumzo ya nyuklia, Marekani kwanza ilitoa ruhusa kwa uchokozi haramu wa utawala wa Kizayuni na kisha ikajiunga na kampeni hii haramu kwa kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran kwa mabomu.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza mara kwa mara kwamba, kama mwanachama wa Mkataba wa Kutosambaza Urani ina haki ya kurutubisha urani na haitaacha haki hii.

Wakati wa hatua za kivamizi za utawala wa Kizayuni na Marekani, vituo vitatu vya nyuklia vya Iran ambavyo vipo chini ya mfumo wa ulinzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki vilishambuliwa. Grossi, akiwa Mkurugenzi Mkuu Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, mpaka sasa hajalaani waziwazi kitendo hiki haramu na ametaka tu kufanyika ukaguzi wa vituo hivyo.

Grossi ameliambia gazeti la Financial Times kwamba, wakaguzi wa IAEA wamekuwa wakisubiri kwa miezi kadhaa ili kuruhusiwa kufika katika maeneo hayo matatu muhimu ya nyuklia yaliyoshambuliwa. Viongozi wa Iran wanasisitiza kuwa, IAEA haina haki ya kutaka kukagua vituo vilivyoshambuliwa.

 

Hii ni katika hali ambayo Iran imetoa uwezekano wa kutembelea vituo vingine ambavyo havikuharibiwa katika mashambulizi hayo na imetangaza kwamba haitaruhusu ukaguzi wa maeneo yaliyoharibiwa hadi Shirika hilo litakapofafanua msimamo wake kuhusu utawala wa Kizayuni na Marekani na kufafanua mfumo wa hali ya baada ya vita ya vituo vilivyo chini ya usimamizi wa shirika hili. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kwamba msingi wa ushirikiano na maingiliano na shirika hilo ni sheria iliyoidhinishwa na Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran), ambayo imelitambulisha Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kama mhusika wa jambo hili.

Matamshi ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, kuhusu kutambua haki ya Iran ya kurutubisha urani licha ya ombi lake la ukaguzi wa vituo vyake vya nyuklia yamezingatiwa mno na duru mbalimbali. Msimamo huu unapaswa kutathminiwa katika muktadha wa sheria za kimataifa, hali halisi ya kiufundi ya mpango wa nyuklia wa Iran, na juhudi za kidiplomasia za kupunguza mvutano.

Mojawapo ya sababu muhimu zaidi za matamshi haya ni msingi wa kisheria katika Mkataba wa Kutosambaza Silaha za Nyuklia. Kulingana na mkataba huu, nchi wanachama, ikiwa ni pamoja na Iran, zina haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani. Urutubishaji urani katika ngazi ya raia, ikiwa utasimamiwa na kukaguliwa kimataifa, unatambuliwa kama sehemu ya haki hii. Kwa mtazamo huu, matamshi ya Grossi yanaweza kuonekana kama msisitizo juu ya mfumo wa kisheria uliopo unaotofautisha kati ya matumizi ya amani na shughuli za kijeshi.

Sababu nyingine ni uhalisia wa kiufundi na kisiasa. Mpango wa nyuklia wa Iran umefikia hatua katika miaka ya hivi karibuni ambapo uwezo wa urutubishaji umeimarishwa tena kwa kutegemea wataalamu wake wa ndani ya nchi. Katika mazingira kama haya, kupuuza ukweli huu au kukataliwa kabisa na taasisi za kimataifa kunaweza kuzuia kupiga hatua mazungumzo na ushirikiano. Hapana shaka kuwa, kutambua haki ya urubishaji urani, ni juhudi za kuunda msingi wa busara wa mazungumzo na kuzingatia uwazi na ufuatiliaji badala ya makabiliano.

 

Kwa upande mwingine, msimamo huu unaweza kuwa ishara ya juhudi za shirika hilo kudumisha msimamo wake unaojulikana kama wa "kutoegemea upande wowote." Ingawa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki linalazimika kutofautisha kati ya masuala ya kiufundi na mashinikizo ya kisiasa, lakini mara kwa mara wakala huo umechukua misimamo na hatua hasi kuhusu suala la shughuli za nyuklia za amani za Iran chini ya mashinikizo ya madola ya Magharibi na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa muktadha huo, matamshi ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimata wa Nishati ya Atomiki (IAEA) yanaweza kuonekana kama sehemu ya mkakati mpana wa kidiplomasia wa kupunguza mvutano. Hii inaeleweka, hasa baada ya ripoti kwamba Washington imekubali kiwango cha urutubishaji urani nchini Iran katika mazungumzo ya hivi karibuni. Kwa maneno mengine, msimamo mpya wa Grossi unapaswa kutathminiwa katika muktadha wa msimamo wa hivi karibuni wa Marekani. Kukubali haki za nyuklia za Iran kwa kiwango kinachozingatia kanuni kunaweza kujenga uaminifu na kufungua njia ya makubaliano mapya au mifumo iliyoimarishwa ya ufuatiliaji. Hapana shaka kuwa, utendaji huu unasisitiza usimamizi na ufuatiliaji badala ya kujikita tu katika mbinyo na mipaka.