Rais wa mpito wa Venezuela: Maduro bado ndiye rais halali
https://parstoday.ir/sw/news/world-i136596-rais_wa_mpito_wa_venezuela_maduro_bado_ndiye_rais_halali
Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez, amesema kwamba anaongoza nchi hiyo kwa kuzingatia vifungu vya Katiba, akikanusha madai kwamba Marekani inaendesha Venezuela, huku akisisitiza kwamba Nicolas Maduro anasalia kuwa rais halali wa jamhuri hiyo.
(last modified 2026-02-14T02:22:38+00:00 )
Feb 14, 2026 02:22 UTC
  • Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez
    Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez

Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez, amesema kwamba anaongoza nchi hiyo kwa kuzingatia vifungu vya Katiba, akikanusha madai kwamba Marekani inaendesha Venezuela, huku akisisitiza kwamba Nicolas Maduro anasalia kuwa rais halali wa jamhuri hiyo.

Katika mahojiano yake na NBC News, Rodríguez ameeleza kwamba ameanza majukumu yake kama rais wa mpito kwa mujibu wa Katiba ya Venezuela, akisema: "Ninaweza kuthibitisha kwamba ninaongoza Jamhuri ya Venezuela kama ilivyoainishwa waziwazi na Katiba."

Rodríguez amesisitiza kwamba Nicolas Maduro, ambaye alitekwa nyara na jeshi la Marekani tarehe 3 Januari mwaka huu, anaendelea kuwa rais halali wa nchi hiyo, licha ya matukio ya hivi karibuni katika uwanja wa kisiasa.

Kuhusu uwezekano wa kiongozi wa upinzani, María Corina Machado, kurudi Venezuela, Delcy Rodríguez amehoji sababu za "makelele mengi" yanayoibuliwa kuhusiana na Machado, akisisitiza kwamba kurudi kwake kutalazimu awajibishwe kisheria ndani ya nchi.

Ameongeza kuwa Machado anatakiwa kuelezea sababu za wito wake wa uvamizi wa kijeshi dhidi ya Venezuela na kuwekwa vikwazo dhidi ya nchi hiyo, pamoja na msimamo wake kuhusu operesheni ya kijeshi ya Marekani mwanzoni mwa Januari mwaka huu.

Tarehe 3 mwezi Januari, Marekani iliivamia Venezuela na kumteka nyara Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro na mkewe, Cilia Flores.

Siku chache baada ya hujuma hiyo iliyokiuka sheria za kimataifa, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Venezuela alisema idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio la Marekani ilipindukia watu 200.