Spika Qalibaf akutana na Sultani wa Oman kufuatia mazungumzo ya Uswisi
-
Spika Qalibaf akizungumza na Sultani wa Oman, Muscat.
Spika wa Bunge la Iran ambaye pia ni mkuu wa timu ya mazungumzo na Marekani, Mohammad Baqer Qalibaf, amekutana na Sultani Haitham bin Tariq wa Oman jijini Muscat, ambapo wamejadili uhusiano wa nchi mbili na matukio ya hivi karibuni kuhusu Mkataba wa Maelewano (MoU) kati ya Tehran na Washington.
Akiongoza ujumbe wa Iran, Qalibaf amejadiliana na Sultani Haitham katika Ikulu ya al-Baraka jana Jumanne kuhusu mbinu za kuimarisha ushirikiano kati ya Tehran na Muscat, pamoja na mipango ya usimamizi wa Lango Bahari la Hormuz.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman kupitia mtandao wa kijamii wa X, pande hizo mbili zimejadili matukio ya hivi punde kuhusiana na mazungumzo kati ya Iran na Marekani.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Sultani Haitham ametangaza uunga mkono wake kwa mazungumzo hayo na kuelezea matumaini yake kwamba yatafanikiwa kupata “suluhisho la amani na la kudumu kwa masuala yote yaliyosalia,” ikiwa ni pamoja na kurejea usafirishaji wa majini kupitia Lango Bahari la Hormuz, faili la nyuklia na changamoto nyingine zinazohusiana na hayo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Qalibaf amewasilisha salamu za Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, kwa Sultani Haitham, huku akiitakia Oman na wananchi wake “maendeleo na ustawi endelevu.”
Ujumbe wa Iran umepongeza, kwa niaba ya uongozi, serikali na wananchi, msimamo wa busara wa Oman chini ya uongozi wa Sultani Haitham, pamoja na mchango chanya wa Muscat katika kuunga mkono majadiliano, kupunguza mivutano na kuzidisha fursa za amani na utulivu katika kanda hii.
Kwa upande wake, Sultani Haitham bin Tariq alimuomba Qalibaf kufikisha salamu zake kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, na kwa Rais Pezeshkian, akiliombea usalama, utulivu, na ustawi wa kudumu taifa la Iran.
Qalibaf, ambaye aliwasili Muscat Jumatatu jioni kufuatia mazungumzo kati ya Iran na Marekani nchini Uswisi na kusimama kwa muda mfupi mjini Tehran, anaongoza ujumbe wa Iran kwa ajili ya mashauriano ya pamoja na maafisa wa Oman kuhusu usimamizi wa Lango Bahari la Hormuz.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amefuatana na Spika wa Bunge katika ziara hiyo rasmi. Mara baada ya ujumbe huo kuwasili Muscat, Iran na Oman ziliunda kamati ya pamoja kwa ajili ya kujadili suala la usimamizi wa Lango la Bahari la Hormuz.