Admeri Shamkhani asisitiza: Mpango wa makombora wa Iran hautajadiliwa katu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136542-admeri_shamkhani_asisitiza_mpango_wa_makombora_wa_iran_hautajadiliwa_katu
Uwezo wa makombora ya balestiki ya Iran ni "mstari mwekundu" ambao hautawekwa katu kwenye meza ya mazungumzo. Hayo yameelezwa na afisa wa ngazi ya juu wa ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-02-12T06:31:46+00:00 )
Feb 12, 2026 06:31 UTC
  • Admeri Shamkhani asisitiza: Mpango wa makombora wa Iran hautajadiliwa katu

Uwezo wa makombora ya balestiki ya Iran ni "mstari mwekundu" ambao hautawekwa katu kwenye meza ya mazungumzo. Hayo yameelezwa na afisa wa ngazi ya juu wa ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Admeri Ali Shamkhani, ambaye anahudumu kama Katibu wa Baraza la Ulinzi la Iran, taasisi tanzu ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran (SNSC), ametangaza msimamo huo pembeni ya maandamano ya maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Februari 11.

Shamkhani ametoa kauli hiyo wakati Marekani inaendelea kushinikiza kupanuliwa wigo wa mazungumzo yanayoendelea ya nyuklia ili kujumuisha mpango wa makombora ya Iran.

Matamshi ya Katibu wa Baraza la Ulinzi yametafsiriwa kuwa ni mjibizo wa moja kwa moja kwa wito mpya wa serikali ya Donald Trump ya kutaka mpango wa makombora wa Iran uwe na mipaka maalumu.

Wakati Iran imeonyesha nia ya kujadili shughuli zake za nyuklia mkabala wa kupunguziwa vikwazo, imekuwa ikisisitiza kutenganishea mpango wake wa makombora ya ulinzi na mazungumzo hayo.

Admeri Shamkhani amesema, chokochoko zozote za kijeshi, bila kujali ukubwa wake, zitakabiliwa na jibu kamili.

Ameionya Marekani kwamba hata kama itafanya "shambulio la kiwango maalumu" dhidi ya maslahi ya Iran, Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu vimeshaashiria wazi kupitia taarifa rasmi na kwa kuonyesha nguvu zake kwenye medani kwamba uchokozi wowote utachukuliwa kama uanzishaji wa vita kamili.

Shamkhani amesema njia pekee ya kimantiki ya kusonga mbele kwa Magharibi ni kufuatilia "mazungumzo ya dhati" na kuachana na "tabia za maonyesho na propaganda" ambazo zinalenga tu kuvuruga utulivu wa eneo.../