Jeshi Mali lamuangamiza kinara wa Daesh katika eneo la Sahara
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128610-jeshi_mali_lamuangamiza_kinara_wa_daesh_katika_eneo_la_sahara
Jeshi la Mali limetangaza kuwa limemuua Souleymane Ag Bakawa, mmoja wa viongozi wa kundi la kigaidi la Daesh katika eneo pana la Sahara, wakati wa operesheni ya kiusalama katika eneo la Tinfadimata, kaskazini mwa Mali.
(last modified 2026-02-02T06:45:47+00:00 )
Jul 22, 2025 04:37 UTC
  • Jeshi Mali lamuangamiza kinara wa Daesh katika eneo la Sahara

Jeshi la Mali limetangaza kuwa limemuua Souleymane Ag Bakawa, mmoja wa viongozi wa kundi la kigaidi la Daesh katika eneo pana la Sahara, wakati wa operesheni ya kiusalama katika eneo la Tinfadimata, kaskazini mwa Mali.

"Mtu huyu aliyeogopwa sana, aliongoza kundi la IS eneo la Sahara, genge linalojulikana pia kama "Soldat," na linalotambulika kwa kueneza taharuki na ugaidi katika mji wa Menaka na maeneo jirani," jeshi la Mali limesema katika taarifa ya jana Jumatatu.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, gaidi huyo alihusika moja kwa moja katika utekaji nyara kadhaa wa raia na mauaji yaliyolenga wanajeshi wa Mali na raia wasio na hatia.

Haya yanaripotiwa huku wanajeshi wa Mali wakishadidisha operesheni zao dhidi ya magenge ya kigaidi. Jeshi la Mali lilitangaza juzi Jumapili habari ya kuangamizwa magaidi zaidi ya 70 katika operesheni mbili za kiusalama katika maeneo ya kaskazini na katikati mwa nchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo, operesheni ya kwanza ilifanyika Julai 15 kwa uratibu wa vikosi vya anga kutoka Muungano wa Nchi za Sahel, na kupelekea kuangamizwa karibu magaidi 40 katika eneo la Anderamboukan, kaskazini mwa nchi hiyo.

Operesheni ya pili iliyofanywa siku mbili baadaye na wanajeshi wa Mali, ilisababisha uharibifu wa kambi ya vifaa na mafunzo ya kigaidi katika eneo la Niono katikati mwa Mali, na vifo vya magaidi wapatao 30, taarifa hiyo imeongeza.

Aidha mapema mwezi huu, magaidi wengine zaidi ya 80 waliuawa katika mashambulizi ya jeshi la Mali yaliyolenga maeneo kadhaa ya katikati na magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.