Malaysia yasisitiza msimamo wake wa kuendelea kuwafukuza Waisraeli
https://parstoday.ir/sw/news/world-i140168-malaysia_yasisitiza_msimamo_wake_wa_kuendelea_kuwafukuza_waisraeli
Waziri wa Ulinzi wa Malaysia, Mohamed Khaled Nordin, amesisitiza kuwa serikali ya nchi hiyo itaendelea kuwafukuza raia wa Israel kutoka katika ardhi ya Malaysia, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya sera ya muda mrefu ya Kuala Lumpur ya kutoutambua utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2026-07-26T02:53:08+00:00 )
Jul 26, 2026 02:51 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Malaysia, Mohamed Khaled Nordin
    Waziri wa Ulinzi wa Malaysia, Mohamed Khaled Nordin

Waziri wa Ulinzi wa Malaysia, Mohamed Khaled Nordin, amesisitiza kuwa serikali ya nchi hiyo itaendelea kuwafukuza raia wa Israel kutoka katika ardhi ya Malaysia, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya sera ya muda mrefu ya Kuala Lumpur ya kutoutambua utawala wa Kizayuni wa Israel.

Waziri huyo amesema kuwa, hatua yoyote inayochukuliwa dhidi ya Waisraeli inatekelezwa kwa mujibu wa sera rasmi za Malaysia kuhusu utawala wa Israel.

Alifafanua kuwa hatua za hivi karibuni za kuwafukuza baadhi ya Waisraeli zililenga kuhakikisha kuwa hakuna raia wa Israel waliopo katika kituo kinachojulikana kama Network School, kilichopo eneo la Forest City katika jimbo la Johor.

Kauli hiyo imetolewa baada ya wabunge wanane wa Bunge la Marekani kuutaka utawala wa Washington kupitia upya uhusiano wake wa kiusalama na kiuchumi na Malaysia, kufuatia taarifa kwamba baadhi ya Waisraeli waliingia nchini humo wakitumia pasi za kusafiria za mataifa mengine.

Wabunge hao pia wameitaka serikali ya Marekani kuzingatia kusitisha ufadhili wa mpango wa International Military Education and Training (IMET) kwa vikosi vya jeshi la Malaysia iwapo Kuala Lumpur haitabadilisha msimamo wake ndani ya siku 15.

Aidha, Waziri wa Ulinzi wa Malaysia alipuuza wasiwasi kwamba msimamo huo unaweza kuathiri ufadhili wa mpango wa Elimu na Mafunzo ya Kijeshi ya Kimataifa (IMET), akisisitiza kuwa sera ya Kuala Lumpur kuhusu utawala wa Kizayuni haijabadilika kwa miaka mingi. Alisisitiza: "Sera yetu ni kutoutambua utawala wa Israel; hilo ndilo msimamo wetu."

Malaysia, ambayo ni mtetezi mkubwa wa harakati za kupigania ukombozi za Palestina, haiitambui Israel na inawazuia watu wenye pasipoti za Israel kuingia nchini humo.

Nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Indonesia, Pakistan, Algeria, Iraq, Lebanon, Syria, Yemen, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kadhalika, haziitambui Israel na hazina uhusiano wowote wa kidiplomasia na utawala huo haramu.