Rais wa zamani wa Kongo, Joseph Kabila, apinga vikwazo vya US mahakamani
-
Joseph Kabila
Katika kesi iliyofanyika mahakamani huko Washington, Joseph Kabila ambaye aliongoza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuanzia 2001 hadi 2019 ametaka jina lake liondolewe kwenye orodha nyeusi ya Wizara ya Fedha ya Marekani.
Kabila amesisitiza kuwa kuwekwa jina lake katika orodha ya vikwazo na Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Kigeni ya Marekani (OFAC) mwezi Aprili kulitokana na madai yasiyo na msingi.
Washington inamtuhumu Kabila kuwa amefadhili na kutoa msaada wa kisiasa kwa waasi wa kundi la M23 wa mashariki mwa Kongo wanaoungwa mkono na Rwanda ambao mwaka jana walidhibiti mikoa miwili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hata hivyo Joseph Kabila amesema kwamba serikali ya Marekani haijaweka wazi uhamisho wa fedha au motisha yoyote ya kisiasa aliyoitoa kwa waasi.
Baada ya kuwa uhamisho kwa kujitakia kwa miaka kadhaa Kabila mwaka jana alionekana katika mji wa Goma, miezi michache tu baada ya mji huo kudhibitiwa na waasi.
Mahakama ya kijeshi ya Kongo imemhukumu Joseph Kabila adhabu ya kifo bila yeye kuwepo mahakamani kwa kosa la uhaini na mashtaka mengine kwa mchango wake kwa waasi wa M23.
Vurugu na machafuko yameendelea mashariki mwa Kongo Hata baada ya makubaliano ya amani kati ya Kinshasa na Kigali, huku kila upande ukiutuhumu mwenzake kwa kukiuka makubaliano hayo.