Iran: Mashambulizi yataendelea hadi adui atakapojisalimisha kikamilifu
-
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Mohammad Baqer Zolghadr
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Mohammad Baqer Zolghadr amesema mashambulizi ya vikosi vya jeshi la Iran yataendelea hadi adui atakapojisalimisha kikamilifu na hadi kulipiza kisasi kwa damu ya mashahidi.
Kwa mujibu wa Pars Today ikinukuu Shirika la Utangazaji la Iran (IRIB), Zolghadr katika ujumbe wake amesema kila nguzo ya moshi inayoonekana katika eneo hilo ni ishara ya kulengwa kwa kituo cha kijeshi, kiusalama au kifedha cha Marekani.
Amesema mashambulizi endelevu na yenye malengo yanayofanywa na jeshi shupavu la Iran ni "mijeledi ya hasira ya taifa la Iran lililoamka" dhidi ya mfumo wa utawala wa kibeberu.
Zolghadr ameongeza kuwa mashambulizi hayo yataendelea hadi "kujisalimisha kikamilifu kwa adui na kulipiza kisasi cha damu ya watoto wasio na hatia wa Minab na Lamerd pamoja na wengine waliouawa shahidi kidhulma na majeshi ya kigaidi ya Marekani na Israel."
Huku hayo yakiripotiwa, Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza kuwa, limetekeleza mashambulizi mapya dhidi ya ngome za kijeshi za Marekani nchini Kuwait na Bahrain, huku likitoa onyo kwa raia katika nchi zinazowapa hifadhi wanajeshi wa Marekani kuondoka mara moja na kuwa mbali kwa angalau mita 500 kutoka maeneo yanayotumiwa na wanajeshi hao.