Namna Trump Anavyodhihirisha Hasara ya Vita na Iran kama Mafanikio
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140150-namna_trump_anavyodhihirisha_hasara_ya_vita_na_iran_kama_mafanikio
Kwa kuchapisha orodha ya wahanga wa vita tofauti vya Marekani, Rais Donald Trump amejaribu kudhihirisha mzozo na Iran kama "vita vyenye gharama ya chini, na vilivyofanikiwa" ambapo sasa anajivunia vifo vya wanajeshi 18 wa Marekani walioangamia katika vita vya karibuni.
(last modified 2026-07-25T09:19:56+00:00 )
Jul 25, 2026 09:17 UTC
  • Namna Trump Anavyodhihirisha Hasara ya Vita na Iran kama Mafanikio

Kwa kuchapisha orodha ya wahanga wa vita tofauti vya Marekani, Rais Donald Trump amejaribu kudhihirisha mzozo na Iran kama "vita vyenye gharama ya chini, na vilivyofanikiwa" ambapo sasa anajivunia vifo vya wanajeshi 18 wa Marekani walioangamia katika vita vya karibuni.

Simulizi hii ya Trump imeibua hisia kali kutoka kwa vyama vyote viwili vikuu vya Democratic na Republican, na kwa mara nyingine kuibua swali la msingi kwamba: Je, mafanikio ya vita yanaweza kupimwa kwa idadi ya vifo pekee?

Chuck Schumer, Kiongozi wa chama cha Demokrasia katika Seneti ya Marekani amesema: "Kujivunia vifo vya askari 18 wa Marekani katika vita vya kizembe na haramu ambavyo amevianzisha bila sababu yoyote ya maana ni kilele cha kutokuwa na aibu."

Kwa kulinganisha takwimu za wahanga wa vita vya Vietnam, Korea, Iraq, na Afghanistan na za vita na Iran, Trump amejaribu kuonyesha kwamba makabiliano na Iran ni vita vya "gharama nafuu", na "vilivyofanikiwa." Pamoja na hayo, kile ambacho kimeanikwa wazi na takwimu hizo kabla ya kuwa mafanikio ya kijeshi, ni mgogoro mkubwa zaidi ulioko katika uelewa wa asili wa maana ya vita, ambapo maisha ya binadamu yanashushwa hadhi na kuwa namba tu kwa ajili ya propaganda za kisiasa.

Simulizi hii ya kitoto imekosolewa si na wanachama wa chama cha demokrasia pekee, bali pia na watu wa ndani ya kambi ya Trump mwenyewe. Marjorie Taylor Greene, mbunge wa chama cha Republican, ametafsiri chapisho hilo kama "kujigamba kuhusu vifo vya askari 18 wa Marekani," huku Gavana wa California, Gavin Newsom, akimtaja Trump kama "mtu mdogo na duni" ambaye anapaswa kuwaheshimu wanajeshi. Mitazamo hii inaonyesha kuwa, hata katika mazingira ya mgawanyiko mkali wa kisiasa mjini Washington, jaribio la kupunguza uzito wa vifo vinavyotokana na vita limevuka mstari mwekundu ambao pande zote mbili zinakubaliana kwamba haupaswi kuvukwa.

Swali la msingi hapa ni iwapo mafanikio ya vita yanaweza kupimwa kwa kutumia idadi ya vifo pekee. Taasisi nyingi mashuhuri za uchambuzi wa sera nchini Marekani zinajibu kwa kusema hilo halipasi kufanyika. Shirika la RAND linasisitiza kwamba kipimo cha mafanikio ni kufikia malengo yaliyotangazwa rasmi kisiasa na kijeshi, kudumisha utulivu wa eneo, na kufikia maslahi ya muda mrefu, na sio kupunguza tu vifo na majeruhi. Vile vile, Taasisi ya Brookings imeonya kwamba kutaja idadi ya vifo pekee hupotosha watunga sera na kuwafanya waghafilike na gharama halisi za vita, kama vile kuharibiwa itibari ya kimataifa, mashinikizo ya kiuchumi, kudhoofishwa nguvu ya kuzuia hujuma na kuvurugwa uthabiti wa kikanda.

Wakati huo huo, Majid Nili, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Ujerumani, anasema: "Historia haiandikwi kwa idadi ya vifo bali kwa kina cha taathira." Akitolea mfano shambulio la kinyama la mabomu katika shule ya msingi ya Minab na pia katika ofisi ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika siku ya kwanza ya uchokozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, shambulio lililopelekea kuuawa shahidi huyo na pia wanafunzi 168, amesisitiza kuwa "wakati mwingine, taathira za uchokozi mfupi wa kijeshi hudumu na kubakia zaidi kwenye kumbukumbu kuliko miongo kadhaa ya vita na maelfu ya wahanga." Mtazamo huu hubadilisha maana ya "gharama ya vita" kutoka takwimu dhahania na kuwa uhalisia wa kibinadamu na kihistoria, huku ukionyesha namna tukio lenye uzito wa kipekee linavyoweza kubuni mtazamo wa taifa kuhusu haki na mapambano kwa vizazi vijavyo.

Karne mbili zilizopita, Carl von Clausewitz, mtaalamu mahiri wa masuala ya kijeshi alisema vita ni mwendelezo wa siasa kwa mbinu nyingine, hivyo, matokeo yake yanapaswa kutathminiwa kwa kuzingatia taathira za kisiasa na kimkakati na sio idadi ya wahanga. Kwa mtazamo huu, huenda vita vilivyo na vifo vichache vikawa na taathira kubwa na za kina zaidi kijiopolitiki na kiusalama kuliko vita vinavyosababisha makumi ya maelfu ya vifo.

Taasisi ya Quincy imeonya mara kwa mara kwamba kutegemea nguvu za kijeshi kupita kiasi, bila kujumuisha diplomasia, kunaweza, katika muda mrefu, kuibua mgogoro mkubwa zaidi kuliko vita yenyewe, hata kama idadi ya vifo itakuwa ndogo.

Ukweli ni kwamba uzoefu wa vita vya Vietnam, Iraqi na Afghanistan umetoa somo la pamoja kwa sera za kigeni za Marekani. Hakuna hata moja ya vita hivi vilivyobakia katika kumbukumbu ya kihistoria kutokana na idadi ya wahanga wake, bali vimegeuka kuwa alama ya kufeli Marekani au kudhoofika nguvu zake za kijeshi na hilo bila shaka litokana na taathira zake za kisiasa, kiuchumi na kimkakati. Hivyo, simulizi ya Trump, inayojaribu kupunguza taathira za vita dhidi ya Iran kuwa jedwali la takwimu tu, si tathmini ya kimkakati bali ni jitihada za kipropaganda zinazolenga kudhibiti maoni ya umma.

Historia ya mahusiano ya kimataifa inaonyesha kuwa haitathmini vita kwa idadi ya wahanga, bali kwa taathira zinazoachwa kwa mataifa, uwiano wa nguvu na mifumo ya kieneo,  kigezo ambacho kinatoa changamoto kubwa zaidi kwa simulizi ya Trump kuhusu uchokozi wake dhidi ya Iran.