Araqchi: Ufaransa, Ujerumani na Uingereza hazina mamlaka ya kuhuisha "Snapback Mechanism"
-
Abbas Araqchi
Iran imesema kuwa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza hazina hadhi ya kisheria, kisiasa wala ya kimaadili ya kuhuisha utekelezaji wa kile kinachojulikana kama Snapback Mechanism ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015. Snapback Mechanism ni utaratibu wa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesisitiza msimamo wa Tehran katika barua iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, Mwenyekiti wa Baraza la Usalama na wanachama wake, na kwa Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya (EU) Bi Kaja Kallas.
Araqchi amesisitiza kuwa nchi tatu za Ulaya yaani Ufaransa, Ujerumani na Uingereza (E3) zimeunga mkono uvamizi wa Israel dhidi ya Iran, zilipinga sheria za msingi za makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kupuuza utekeleza majukumu yao kwa mujibu wa makubaliano hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Tehran ilitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa JCPOA licha ya Marekani kujitoa kwa upande mmoja katika makubaliano hayo, hata hivyo Ufaransa, Ujerumani na Uingereza ziliunga mkono kile kinachofahamika kama mashinikizo ya kiwango cha juu ya Washington dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
"Hatua yoyote ya kurejesha maazimio yaliyosimamishwa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni batili", amesema Sayyid Abbas Araqchi.
Amesisitiza kuwa E3 hazipaswi kupewa mwanya wa kudhoofisha imani ya Baraza la Usalama la UN kwa kutumia vibaya maazimio ya baraza hilo.