Kiongozi Muadhamu: Uimara wa Hizbullah ni ujumbe kwa mataifa huru
-
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, ameisifu harakati ya Hizbullah ya kwa msimamo wake thabiti na usioyumba katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema, kuwa uimara wa harakati hiyo ya Lebanon ni ujumbe wenye nguvu wa ukombozi kwa mataifa yaliyodhulumiwa duniani kote.
Akijibu barua kutoka Hizbullah ambapo harakati hiyo ilisisitiza utii na uaminifu wake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza harakati hiyo kwa kusimama “kama jabali lisilotikisika” mbele ya “uchokozi wa kinyama” wa Israel na waungaji mkono wake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Kiongozi, ustahimilivu wa Hizbullah sasa umegeuka kuwa “ujumbe wa kutia hamasa kwa mataifa huru ya dunia katika harakati zao za kujikomboa dhidi ya dhulma na ukandamizaji unaotekelezwa na Uistikbari wa Kimataifa na vibaraka wake.”
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewasifu makamanda na wapiganaji wa Hizbullah kwa “subira, uvumilivu na ustahimilivu” wao katika kutetea misingi ya Muqawama wa Kiislamu, akisema ujumbe wao unaakisi imani imara katika ahadi za Qur’ani Tukufu na urithi wa Imam Khomeini pamoja na Kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.
Amesema kuongezeka kwa hisia za kuchoshwa na Marekani na utawala wa Israel katika medani ya kimataifa kunamaanisha “hakuna njia nyingine isipokuwa jihadi na muqawama”, huku akieleza yakini kuwa uthabiti katika njia hiyo hatimaye utaleta “ushindi wa Mwenyezi Mungu uliyoahidiwa.”
Ayatullah Khamenei pia aliwapongeza wananchi wa Lebanon, hasa wakazi wa kusini mwa nchi hiyo, akisema subira yao, kujitolea kwao na uungaji mkono wao vimekuwa na nafasi ya msingi katika kuendeleza Muqawama.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza tena kuwa Jamhuri ya Kiislamu inaona kuwahami wapiganaji wa Hizbullah kuwa “jukumu lake la kimkakati.”
Ayatullah Khamenei amesema Iran imeweka bayana kwamba kulindwa kwa ukamilifu wa ardhi ya Lebanon na kukomeshwa kabisa, bila masharti, kwa uchokozi wa Israel ni sharti kuu kwa makubaliano yoyote yanayolenga kumaliza vita vya kulazimishwa na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia alitoa heshima kwa mashahidi wa Hizbullah, akiwemo Katibu Mkuu wa zamani, Sayyid Hassan Nasrallah, akisema wao wameibadilisha harakati hiyo “kutoka mche mdogo hadi kuwa mti mkubwa na imara” na kuiletea Lebanon heshima katika ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amewaombea dua wapiganaji wa Hizbullah, maveterani wake, waliolazimika kuhama makazi yao, pamoja na familia za mashahidi, akieleza matumaini kwamba hatimaye watapata ushindi.
Ujumbe wa Kiongozi ulitolewa kujibu barua ya awali ya ahadi ya utii iliyoandikwa na wapiganaji wa Hizbullah, ambao waliapa kubaki waaminifu kwa Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei na kuendelea katika njia ya Shahidi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.
Katika barua hiyo, wapiganaji hao waliahidi “kuendelea katika njia ileile ya heshima na izza” na wakaapa kusimama pamoja na Ayatullah Khamenei kwa “msimamo usioyumba”, wakisema wataendelea kuwa waaminifu kama walivyokuwa kwa kiongozi wao shahidi, na hawataogopa lawama yoyote “katika njia ya Allah.”
Wapiganaji wa Muqawama walimhakikishia Ayatullah Khamenei kwamba ndani yao hatapata “chochote isipokuwa utiifu, azma isiyovunjika ya kufikia ushindi, na mapenzi ya kufa shahidi.”